Khatibu wa Swala ya Ijumaa Tehran: Wanaochoma moto Qur’ani kwa hakika wanajichoma moto wao wenyewe

Khatibu wa Swala ya Ijumaa mjini Tehran ameeleza kuwa, wale wanaochoma moto nakala za Qur’ani Tukufu kwa hakika wanajichoma moto wao wenyewe na kusema: Si jambo rahisi kwa kila mtu kujua hakika ya Qur’ani ambayo ni roho na rehema ya Mwenyezi Mungu, na kufanya ukaidi dhidi ya neno la Mungu ni ishara ya roho ya kishetani.

Hujjatul-Islam Kazem Seddiqi, khatibu wa Swala ya Ijumaa mjini Tehran ameashiria watu wanaochoma moto nakala za Qur’ani katika baadhi ya nchi za Ulaya na kusema: “Hawa viumbe waovu wanaoichoma moto Qur’ani hawana njia ya kuifikia na kuifahamu Qur’ani na kwa hakika wanajichoma moto wao wenyewe.”

Hujjatul-Islam Kazem Seddiqi amesema kuwa uchamungu ndio njia ya uokovu, na ukosefu wa uchamungu ndio sababu ya kuangamia na kuongeza kuwa: “Uchamungu ni nyumba imara, na mtu anayeishi katika ngome hii atasalimika na shari ya nafsi inayoamrisha maovu na yenye kiburi; lakini kinyume chake, ukosefu wa taqwa na uchamungu huwa sababu ya kuangamia kwa mwanadamu.

Vitendo viovu vya kuvunjia heshima kitabu kitukufu cha Qur’ani vimelaaniwa na jamii ya kimataifa akiwemo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, ambaye ametangaza mshikamano wake na jamii ya Waislamu na kulaani hatua yoyote ya hujuma na propaganda chafu dhidi ya Uislamu na inayochochea mivutano.

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis pia amelaani vitendo vya kuvunjiwa heshima Qur’ani Tukufu katika nchi za Sweden na Denmark na kusisitiza kuwa, vitendo hivyo vya kudhalilisha matukufu ya kidini havina tofauti na ukatili.

Papa amesema ameghadhabishwa na kukerwa na vitendo vya kuvunjiwa heshima Qur’ani Tukufu huko nchini Sweden na Denmark, huku akitilia mkazo suala la wafuasi wa dini mbalimbali kuishi pamoja kwa amani na maelewano, sanjari na kupinga misimamo na mitazamo ya kufurutu mipaka.

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani amesema kuwa, uhuru wa maoni na kujieleza haipasi kuonekana kama idhini ya kitendo hicho cha fedheha cha kuvunjia heshima matukufu ya dini nyingine.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *