Huku baadhi ya nchi za Afrika Magharibi zikijiandaa kuingia kijeshi nchini Niger ‘kurejesha’ utawala wa kikatiba, Waziri Mkuu wa nchi hiyo aliyepinduliwa pamoja na serikali ya Rais Mohamed Bazoum wa nchi hiyo ametoa mwito wa kufanyika mazungumzo ili kuhitimisha mzozo huo.
Ouhoumoudou Mahamadou ametoa mwito huo katika mahojiano na shirika la habari la Reuters akiwa mjini Paris, Ufaransa na kuongeza kuwa, anatumaini diplomasia itatumika kuupatia ufumbuzi mgogoro huo wa uongozi nchini kwake, kabla ya kumalizika makataa ya wiki moja iliyotolewa na Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) kwa wanajeshi waliofanya mapinduzi.
Mahamadou ambaye alikuweko mjini Rome wakati wa mapinduzi hayo ya kijeshi ya mwishoni mwa mwezi uliopita ameeleza kuwa, “Tungali tuna matumaini. Tunataraji Rais Bazoum ataachiwa huru na kurejeshwa madarakani, na taasisi zote zilizovunjwa zitahuishwa kikamilifu.”
Hii ni katika hali ambayo, wakuu wa kijeshi wa Afrika Magharibi wamekubaliana na mpango wa kuingilia kijeshi Niger wakati muda waliowapa wanajeshi waliofanya mapinduzi utakapomalizika.
Kamishna wa ECOWAS, Abdel-Fatau Musah amenukuliwa na vyombo vya habari vya kieneo na kimataifa akisema mjini Abuja Nigeria kwamba: “Hatimaye mambo yote yanayohusiana na uingiliaji wa aina yoyote ile yamefanyiwa kazi; ikiwa ni pamoja na rasilimali zinazohitajika pamoja na jinsi na lini tutapeleka kikosi (huko Niger).”
Jumapili iliyopita, ECOWAS iliwapa wanajeshi waliompindua Rais Mohamed Bazoum muda wa wiki moja kumrejesha madarakani kiongozi huyo au wakubali kukabiliana na matumizi ya nguvu dhidi yao. Wanajeshi hao walifanya mapinduzi hayo ya kijeshi terehe 26 mwezi uliopita wa Julai.
Waziri Mkuu aliyepinduliwa wa Niger amesema amekuwa akifanya mawasiliano na Rais Bazoum, na kuongeza kwamba usalama wa kiongozi huyo aliyepinduliwa upo mikononi mwa jumuiya ya ECOWAS.