Kiongozi wa upinzani Senegal alazwa hospitalini baada ya kususia kula kwa wiki nzima

Kiongozi wa upinzani nchini Senegal ambaye amekuwa kwenye mgomo wa kula akipinga kuwekwa kizuizini, amelazwa hospitalini. Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na wafuasi wake.

Ousmane Sonko alilazwa katika Hospitali Kuu iliyoko kwenye mji mkuu wa Senegal, Dakar jana Jumapili, kulingana na taarifa kutoka chama chake ambacho sasa kimevunjwa na kupigwa marufuku cha Wazalendo wa Senegal, Patriots of Senegal (PASTEF).

Sonko mwenye umri wa miaka 49, alikamatwa Julai 28 akishtakiwa kwa tuhuma za kupanga uasi, kudhoofisha usalama wa serikali na kutoa ushirikiano wa kihalifu kwa kundi moja la kigaidi.

Kiongozi huyo mashuhuri wa upinzani alianza mgomo wake wa kususia kula siku mbili baadaye.

PASTEF imebainisha katika taarifa yake kwamba Sonko alikuwa amelazwa kitengo cha uangalizi maalumu na imesisitiza kuwa mamlaka za dola ndizo zinazobea dhima ya “kuwajibika” kuhusiana na hali yake.

“Kabla ya kufungwa, alikuwa na afya njema na hakuwa akijulikana kuwa na maradhi yoyote”, imeongeza taarifa hiyo.

Cire Cledor Ly, mmoja wa mawakili wa Sonko, amevithibitishia vyombo vya habari taarifa za kulazwa hospitalini mwanasiasa huyo lakini hakueleza chochote kuhusiana na hali yake.

Serikali ya Senegal hadi sasa haijatoa maelezo yoyote juu ya suala hilo.

Sonko, ambaye alishika nafasi ya tatu katika uchaguzi wa rais wa nchi hiyo ya Afrika Magharibi mwaka 2019, anapendwa na vijana wa nchi hiyo.

Kukamatwa kwake na kuvunjwa kwa chama chake kulizusha maandamano mabaya mjini Dakar wiki iliyopita. Watu wasiopungua wawili walifariki katika machafuko hayo na wengine kadhaa walijeruhiwa.

Wafuasi wa Sonko wanasisitiza kuwa mashtaka dhidi yake ni sehemu ya njama za serikali kumzuia asigombee katika uchaguzi wa urais wa 2024…/

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *