Ikiwa Agosti 15 2023 ni miaka miwili tangu kundi la Taliban lilipotwaa mamlaka nchini Afghanistan, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk amewakumbusha wakuu wa Taliban kwamba Afghanistan, kama Taifa, lina wajibu chini ya sheria za kimataifa kuheshimu, kudumisha na kukuza haki za watu wote bila ubaguzi.
Taarifa iliyotolewa na ofisi ya Haki za binadamu jijini Geneva Uswisi OHCHR imemnukuu Türk akisema kuwa “Tunaendelea kusikitishwa sana na hali ya haki za binadamu, hususan vikwazo vikali vilivyowekwa kwa wanawake na wasichana, ambao haki zao za kupata elimu na kazi, uhuru wao wa kutembea na kushiriki katika maisha ya kila siku na ya umma umeharibiwa na mfululizo wa amri za kibaguzi. iliyotolewa tangu kuchukuliwa kwa mamlaka hiyo.”
Wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa kutoka ofisi ya Haki za Kibinadamu wanaendelea kufanya kazi nchini Afghanistan wakifuatilia, kuweka kumbukumbu na kutetea masuala mbalimbali ya haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na haki za wanawake na wasichana, uhuru wa kimsingi, ulinzi wa raia katika migogoro ya silaha na haki za wafungwa.
Mkuu huyo wa OHCHR amesema wanaendelea kushirikiana na mamlaka husika kuhusu masuala hayo ya haki na kuwakumbusha wajibu wao chini ya sheria za kimataifa za haki za binadamu. “Pia tunakutana na mashirika ya kiusalama kuhusu kesi binafsi za ukiukaji wa haki za binadamu na kutembelea magereza kukutana na wafungwa”.
Kamishna Mkuu ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kutowasahau watu wa Afghanistan, ambao pamoja na kukabiliwa na vikwazo vikali vya haki zao za binadamu, wanaishi katika hali mbaya ya kibinadamu na kiuchumi.
“Hakuna Waafghanistan ambao hawajaguswa kwa namna fulani na ghasia na migogoro ya miongo minne iliyopita.”
Waathirika na familia zao nchini Afghanistan wanaendelea kutafuta haki, uwajibikaji na wakati mwingine, msaada wa kuokoa maisha.