Thomas West, mjumbe maalumu wa Marekani katika masuala Afghanistan amedai kuwa, Washington ina wasiwasi na suala la kuongezeka hujuma na mashambulio ya makundi yenye mfungamano na kundi la Daesh na uwepo wenye kuendelea wa mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda.
Faraan: Viongozi wa Marekani wanaamini kuwa, kundi la Daesh linaweza kupata uwezo wa kutekeleza mashambulio nje ya Afghanistan katika kipindi cha miezi 6 hadi 12 ijayo na mtandao wa al-Qaeda na unaweza kufanya hivyo katika kipindi cha mwaka mmoja hadi miwili ijayo.
Madai ya mjumbe na mwakilishi maalumu wa Marekani katika masuala ya Afghanistan kuhusiana na wasiwasi wa nchi yake wa kupanuka wigo wa mashambulio ya kundi la kigaidi la Daesh nchini Afghanistan na uwezekano wa magaidi hayo kutekeleza mashambulio ya kigaidi nje ya Afghanistan ni ya kushangaza mno hasa kwa kutilia maanani mchango na nafasi ya Washington katika kuundwa na kupata nguvu kundi hilo la kigaidi.
Kimsingi ni kuwa, Marekani haiwezi kuficha kuhusika kwake katika kudhihiri na kupata nguvu kundi hilo. Awali kundi la kigaidi la Daesh liliundwa kwa kushirikisha mabaki ya chama cha Baath cha Iraq, masalafi na matakfiri waliokuwa wamekusanywa Iraq kutoka katika maeneo mbalimbali ya dunia. Kwa haraka mno kundi hilo lilipanua wigo wa harakati zake katika nchi za Iraq na Syria.
Marekani ikiwa kinara wa Magharibi ikishirikiana na washirika wake wa Kimagharibi na Kiarabu ilichukua hatua ya kuyaunga mkono na kuyapatia misaada ya hali na mali makundi ya kigaidi na kitakfiri likiwemo kundi Daesh. Lengo la Marekani lilikuwa ni kuiondoa madarakani serikali halali ya Rais Bashar al-Assad nchini Syria sambamba na kudhoofisha mhimili wa muqawama. Kwa muktadha huo, Marekani iliyatumia makundi hayo ya kigaidi kama wenzo wa kufikia malengo yake.
Rais wa wakati huo wa Marekani Donald Trump alisema katika hotuba yake ya kampeni xza uchaguzi kuhusiana na kuhusika moja kwa moja aliyekuwa Rais wa Marekani Barack Obama na Hillary Clinton, aliyekuwa Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani katika kuanzishwa kundi la kigaidi la Daesh. Akihutubia mkutano wake wa kampeni, Trump alitangaza wazi Januari mwaka 2016 kwamba, Hillary Clinton na Barack Obama ndio walioaanzisha kundi la kigaidi la Daesh. Kwa hakika matamshi ya Trump yaliunga mkono tuhuma alizokuwa akikabiliwa nazo Obama ambazo zilielekezwa kwake mara chungu nzima na viongozi wa mataifa mbalimbali ya dunia akiwemo Rais Vladimir Putin wa Russia kuhusiana na kuhusika moja kwa moja Ikulu ya Marekani White House katika kuanzishwa Daesh na vitendo vya kigaidi vya kundi hilo.
Mwaka 2011 hadi 2014, Marekani ililipatia himaya na uungaji mkono mkubwa kundi la kigaidi la Daesh na kuwa na nafasi kuu ya kuwafikishia magaidi hao suhula na misaada ya kilojistiki na kifedha. Baada ya operesheni za Daesh nchini Iraq na kufanikiwa kundi hilo kudhibiti sehemu kubwa ya maeneo ya ardhi ya nchi hiyo, serikali ya Marekani chini ya uongozi wa Barack Obama ikaazimia kulidhibiti kundi hilo. Kwa utaratibu huo mwaka 2014 Marekani ikaanzisha kile kilichojulikana kama muungano wa kimataifa dhidi ya Daesh. Hata hivyo lengo hasa la Marekani lilikuwa ni kulifanya kundi la Daesh libakie lakini katika fremu ya kudhibitiwa ili kwa njia hiyo iweze kulitumia kama wenzo wa mashinikizo ya kufikia malengo yake.
Kuhusiana na Afghanistan pia, katika miaka ya hivi karibuni Marekani ikiwa na mipango iliyoratibiwa imekuwa ikiwaunga mkono wapiganaji wa Daesh hususan kaskazini mwa Afghanistan. Viongozi wa Russia wamesisitiza mara kadhaa kwamba, Marekani ikiwa na nia ya kufikia malengo yake, ilikuwa ikitoa misaada ya kilojistiki na kisilaha kwa wapiganaji wa Daesh nchini Afghanistan. Serikali ya Moscow ilisisitiza kwamba, moja ya vyanzo vya himaya ya magaidi mbali na misaada ya moja kwa moja ilikuwa ni misaada ya kijeshi ya Marekani na wanachama wengine wa Shirika la Kijeshi la Magharibi NATO kwa serikali ya wakati huo ya Afghanistan, misaada ambayo haikuwa na udhibiti unaofaa na matokeo yake ikawa ni rahisi kuporwa na kuingia mikononi mwa Daesh.
Baada ya Marekani kuondoka kwa fedheha nchini Afghanistan Agosti mwaka huu, wigo wa mashambulio ya kigaidi nchini humo upamepanuka huku mamia ya raia wasio na hatia wakipoteza roho na maisha yao. Daima Marekani imekuwa ikilitumia kundi la kigaidi al Daesh kama wenzo wa mashinikizo dhidi ya maadui na wapinzani wake hususan Russia, China na Iran; na bila shaka kuimarishwa Daesh nchini Afghanistan hususan katika maeneo yanayopakana na mataifa ya Asia ya Kati kama Tajikistan na Uzbekistan kunafanyika kwa minajili ya kuishinikiza Moscow na Beijing.
Pir-Muhammad Mulla-Zahi, mweledi na mchambuzi wa masuala ya kisiasa anasema: Marekani imejaza pengo la kutokuweko kwake nchini Afghanistan kwa kulitumia kundi la Daesh.
Kwa utaratibu huo siyo tu kwamba, nia ya kweli ya Marekani ya kupambana na kundi la kigaidi la Daesh ni ya kutiliwa shaka, bali imebainika wazi na bayana kwamba, bila ya himaya na uungaji mkono wa Washington hakuna wakati ambao kundi la kigaidi la Daesh lingeweza kuwa na uwezo wa kutekeleza jinai zake.