Sisitizo la Algeria la kutokuwa tayari kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel

Naibu Spika wa Bunge la Algeria Moussa Kharfi ametamka bayana kuwa nchi yake haitoanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel.

Kharfi amesema, kujiingiza utawala wa Kizayuni Kaskazini mwa Afrika kunafanyika kwa lengo la kuwapatia uhalali wa kisiasa maghasibu hao na akasisitiza kuwa: Algeria ingali imesimama dhidi ya uamuzi wa kuanzisha uhusiano, hata kama itabaki peke yake katika msimamo wake huo.

Kuanzishwa uhusiano wa kawaida kati ya Israel na nchi za Kiarabu imekuwa moja ya mihimili ya sera za Marekani katika miaka ya karibuni, sera ambayo ilianza rasmi katika kipindi cha utawala wa Donald Trump. Katika ufanikishaji wa sera hiyo, baadhi ya nchi za Kiarabu kama Muungano wa Falme za Kiarabu (UAE) na Bahrain pamoja na nchi za Kiafrika za Sudan na Morocco zilikubali kufanya mapatano na kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Kizayuni.

Suala la kuanzisha uhusiano wa kawaida lingali linafuatiliwa na kufanyiwa kazi na Israel na Marekani, hususan katika miaka ya karibuni, ambapo Israel imejaribu kupanua uhusiano wake na nchi za Kiafrika kupitia sera ya kujipenyeza katika nchi hizo na kujinufaisha kiuchumi. Ukweli ni kwamba baada ya utawala wa Kizayuni kugonga mwamba kisiasa katika eneo hili la Asia Magharibi, hivi sasa umeamua kulifanya moja ya vipaumbele vyake suala la kupanua uhusiano na kujenga ushawishi ndani ya nchi za Kiafrika. Unachojaribu kufanya utawala bandia wa Israel ni kutumia mbinu ya utoaji ahadi za kiuchumi ili kupata uungaji mkono wa nchi za Kiafrika, hasa zilizo masikini zaidi kwa kutilia maanani kwamba nchi hizo ni watetezi na waungaji mkono wa haki za watu wa Palestina na malengo yao matukufu ya kupigania uadilifu.

Nchi nyingi za Kiafrika ambazo kwa miaka kadhaa ziliatilika na kufisidiwa kwa ukoloni na uvamizi wa nchi za Magharibi zinakosoa vikali sera za kichokozi za utawala dhalimu wa Israel dhidi ya Wapalestina; na licha ya ahadi zote inazotoa Israel, akthari ya nchi hizo hadi sasa hazijawa tayari kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala huo ghasibu hususan nchi kama Algeria na Tunisia ambazo zina sauti na nafasi muhimu miongoni mwa nchi za Kaskazini mwa Afrika. Kuhusiana na suala hilo, Moussa Kharfi, Naibu Spika wa Bunge la Algeria amesisitiza kuwa, nchi yake haitoanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni, hata kama kutofanya mapatano na Israel kutaigharimu na kuihasiri mno nchi hiyo.

Kabla ya hapo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Tunisia, nayo pia ilitangaza kuwa haina nia ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni, na Bunge la Tunisia pia limeeleza kuwa linachunguza sheria mpya iliyopendekezwa ambayo italitambua suala la kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni kuwa ni kosa la jinai.

Ijapokuwa utawala wa Kizayuni ungali unaendelea kutumia mbinu ya kujipenyeza na kuwa na ushawishi mkubwa zaidi ndani ya nchi za Kiafrika ili uweze kunyonya maliasili za nchi hizo, kuzusha hitilafu na mifarakano baina yao, kuziuzia silaha nchi hizo na kushindana na nchi nyingine kama China na Russia kwa ajili ya kuwania mamlaka ya satua katika eneo hilo, lakini inavyoonekana, sera hiyo ya Israel imegonga mwamba licha ya kila hatua inayojaribu kuchukua pamoja na uungaji mkono inaopata kwa utawala wa Biden.

Inavyoonekana, licha ya hatua zote inazojaribu kuchukua Israel na washirika wake, udhalimu na ukatili unaofanywa na utawala huo wa Kizayuni wa kuwaua kidhulma Wapalestina na kukanyaga haki zao si suala ambalo nchi za Afrika zitakuwa tayari kuufumbia macho, kwani hata wananchi wa Sudan na Morocco ambao serikali zao zimekubali kuanzisha uhusiano na Israel wangali wanaendelea kukosoa vikali uamuzi huo na kutaka uhusiano huo uvunjwe…

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *