Mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu umeripotiwa kuyakumba majimbo matatu ya Sudan.
Takriban visa 817 vinavyoshukiwa kuwa maradhi ya kipindupindu vimeripotiwa katika majimbo matatu ya Sudan, vikiwemo vifo 35.
Visa hivyo viliripotiwa katika majimbo ya Gedaref, Kordofan Kusini na Khartoum, tovuti ya habari inayomilikiwa kibinafsi ya al-Rakoba iliripoti, ikinukuu Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO).
Mwanzoni mwa mwezi huuuSudan ilitangaza mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu katika Jimbo la Gedaref baada ya kesi nne kati ya 264 zinazoshukiwa kuthibitishwa na vifo 16 vinavyohusishwa na ugonjwa huo hatari kuripotiwa tangu Septemba 25.
Wiki iliyopita Umoja wa Mataifa ulisema kuwa miezi kadhaa ya migogoro nchini Sudan imewaacha mamilioni ya watu katika hatari ya ugonjwa wa kipindupindu, surua, malaria na magonjwa mengine bila uwezo wa kutosha wa kujizuia.
WHO pia imeonya kwamba maisha ya zaidi ya wagonjwa 9,000 wa figo yako hatarini kutokana na idadi ndogo ya vituo vya kusafisha damu nchini humo.
Kutokana na mapigano makali baina ya makundi mawili hasimu ya jeshi la Sudan yaliyozuka mwezi Aprili 2023, nchi hiyo inakabiliana na idadi kubwa ya watu waliokimbia makwao, milipuko ya magonjwa na utapiamlo, ambao umechangiwa na mvua kubwa na mafuriko.
Mfumo wa afya umeharibiwa kwa mashambulizi yanayolenga vituo vya afya na uhaba wa vifaa tiba na vifaa vingine, wahudumu wa afya na fedha za uendeshaji.
Takriban 70% ya hospitali katika majimbo yaliyoathiriwa na mizozo hazifanyi kazi, huku hospitali na zahanati tendaji katika majimbo ambayo hayakuathiriwa na migogoro zikizidiwa na wimbi la wakimbizi wa ndani.