Rais wa Liberia na mpinzani wake Boakai wakutana tena katika duru ya pili ya urais

Wananchi wa Liberia wanapiga kura leo Jumanne katika duru ya pili ya uchaguzi kati ya Rais George Weah na Makamu wa Rais wa zamani Joseph Boakai baada ya mchuano mkali wa duru ya kwanza ambapo hakuna aliyeweza kupata zaidi ya asilimia 50 ya kura.

Mwanasoka mashuhuri George Weah, 57, aliongoza kwenye duru ya kwanza ya uchaguzi huo mwezi Oktoba, kwa kupata asilimia 43.83 ya kura, na Boakai alipata asilimia 43.44.

Boakai, 78, ni mwanasiasa mkongwe ambaye kuanzia mwaka 2006 hadi 2018 alikuwa naibu wa Ellen Johnson Sirleaf, rais wa kwanza mwanamke barani Afrika kuwa kuchachaguliwa kidemokrasia.

Wachambuzi wanasema tofauti ndogo ya kura kati yao yaani kura 7,126 katika duru ya kwanza na kukosekana mgombea wa tatu mwenye nguvu, ni ishara ya wazi kwamba duru hii ya pili inayofanyika leo, pia itakuwa na mchuano mkali.

Katika uchaguzi wa mwaka 2017 George Weah Weah alishinda kwa zaidi ya asilimia 61 ya kura.

Huu ni uchaguzi wa nne wa rais baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo lakini wa kwanza bila ya kuwepo ujumbe wa Umoja wa Mataifa.

Baadhi ya wapiga kura wamechukizwa na utendaji wa Weah, hasa kuhusu rushwa, kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira kwa vijana, mfumuko wa bei ya chakula na matatizo ya kiuchumi kwa ujumla.

Wafuasi wa chama tawala wanasema hatua ya serikali ya Liberia ya kupasisha sheria mpya mwezi Julai 2022 inayoipa tume ya kupambana na ufisadi mamlaka ya kuendesha mashtaka, ni ushahidi wa jinsi serikali hiyo inavyopiga vita ufisadi. Hata hivyo, wapinzani wanaeleza kuwa maafisa wawili waliogunduliwa ni mafisadi waligombea viti vya ubunge kwa tiketi ya chama tawala.

Rais George Weah anasema, janga la UVIKO-19 na vita vya Russia na Ukraine vimekwamisha pakubwa mipango ya kufufua uchumi ya serikali yake.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *