Rais Hassan Sheikh Mohamud: Wasomali wanataabika na njaa baada ya janga la mafuriko

Rais wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud amesema kuwa, wananchi wa nchi hiyo hivi sasa wanakabiliwa na baa la njaa baada ya mafuriko yaliyoikumba nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Rais huyo wa Somalia amenukuliwa akisema, watu wamekimbia makazi yao, nyumba na mali zimeharibiwa, watu wana njaa, na hilo ndilo tatizo letu hivi sasa, hilo ndilo tunalozingatia.”

Rais Hassan Sheikh Muhamud pia ameelezea wasiwasi wake kuhusu hatari iliyoongezwa ya magonjwa ya milipuko kama vile malaria na kipindupindu.

Mafuriko ya karibuni nchini Somalia yameua watu 29 na kupelekea wengine laki tatu kupoteza makazi.

Tangu mwanzoni mwa mwezi huu, mvua kali zimeikumba Somalia na majirani zake Kenya na Ethiopia, na kusababisha maporomoko ya ardhi na kuzamisha vijiji na mashamba.

Mafuriko hayo yanakuja baada ya Somalia na baadhi ya maeneo ya Ethiopia na Kenya kukumbwa na ukame mkubwa kuwahi kushuhudiwa katika eneo hilo katika miongo minne iliyopita

Maeneo yaliyoathiriwa zaidi ni ya kusini-magharibi mwa taifa hilo lenye watu milioni 17 na ambalo linakumbwa na mizozo mingi ya ndani.

Barabara zisizopitika na magari yaliyokwama ni baadhi tu ya changamoto ambazo wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu wanakabiliana nazo nchini Somalia.

Taasisi za masuala ya kibinadamu za Umoja wa Mataifa zimesema kwamba zimetenga dola milioni 25 za Kimarekani kwa ajili ya kuanza kuwafikishia misaada wananchi walioathiriwa na mafuriko makubwa nchini Somalia. Tayari watu milioni moja na laki mbili wameripotiwa kuathiriwa na mafuriko hayo ya mara moja kwa karne ya nchini Somalia.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *