Idadi ya watu waliokufa kutokana na janga la mafuriko yaliyokumba maeneo kadhaa nchini Kenya imefikia 120.
Ripoti zinasema kuwa, mbali na maafa hayo ya kiroho, maelfu ya makaazi yamesombwa na maji katika baadhi ya maeneo ya Kenya na kuwalazimisha watu kutafuta hifadhi.
Takwimu hizo mpya zimetolewa na afisa wa ngazi ya juu wa wizara ya mambo ya ndani ya Kenya, Raymond Omollo, ambaye pia amesema kaunti 4 za upande wa mashariki mwa nchi hiyo ya Afrika Mashariki ndizo ambazo zimeathirika zaidi na nyingine 10 zimo kwenye hali ya juu ya tahadhari.
Kulingana na afisa huyo, jumla ya nyumba 89,000 zimeharibiwa kwa mafuriko, hali iliyoilazimisha serikali kuanzisha kambi 112 za kuwahifadhi wale walipoteza maakaazi yao kufuatiia mvua kubgwa zilizoambatana na mafuriko.
Juzi Rais William Ruto aliongoza kikao cha dharura cha Baraza la Mawaziri kujadili athari za mafuriko na kuahidi kutoa mabilioni ya shilingi za Kenya kuwasaidia waliokumbwa na maafa.
Aidha akizungumza hivi kkaribunii na maafisa wa idara mbalimbali zinazohusika na kukabiliana na majanga katika Ikulu ya Nairobi Rais William Ruto wa Kenya amesema serikali yake imeweka mipango ya kuwasaidia raia ambao wameathirika na mafuriko yanayoendelea kuripotiwa kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha kwenye kanda ya Afrika Mashariki.
Nchi za Pembe ya Afrika zinaendelea kusumbuliwa na mafuriko yanayosababishwa na mvua kubwa inayoendelea kunyesha katika eneo hilo.
Shirika la “Save the Children” limesema kwenye ripoti yake kwamba makumi ya watu wamefariki dunia na mamia ya wengine wamelazimika kuyahama maeneo yao kutokana na mafuriko katika nchi za Pembe ya Afrika.
Taarifa ya shirika hilo imeongeza kuwa, hali ya hewa ya El Nino imezidisha mvua katika eneo la Pembe ya Afrika na kuziathiri vibaya nchi mbalimbali hasa Somalia, Ethiopia na Kenya.