Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia wakimbizi UNHCR Jumanne limemtangaza Abdullahi Mire mkimbizi wa zamani na mwandishi wa habari ambaye amekuwa kinara wa kupigania haki ya elimu huku akikabidhi vitabu 100,000 mikononi mwa watoto wakimbizi nchini Kenya kuwa ndiye mshindi wa kimataifa wa tuzo ya wakimbizi ya Nansen mwaka huu 2023.
Kamishna Mkuu UNHCR Filippo Grandi, amesema “Abdullahi Mire ni thibitisho hai kwamba mawazo ya mageuzi yanaweza kutoka ndani ya jamii zilizotawanywa. Ameonesha ustadi mkubwa na ukakamavu katika kuimarisha ubora wa elimu ya wakimbizi.”
Mire alizaliwa nchini Somalia, na alikulia katika kambi za wakimbizi za Dadaab nchini Kenya. Hatimaye alipewa makazi mapya Norway, lakini hamu ya kutumikia jamii yake ilimrudisha nyuma alikokulia.
Alipata kazi nchini Kenya kama mwandishi wa habari na kuanzisha Kituo cha Elimu kwa Vijana Wakimbizi, shirika linaloongozwa na wakimbizi wenyewe ambalo limefungua maktaba tatu katika kambi hizo za wakimbizi, maktaba zilizo na vitabu vilivyotolewa bure kama msaada na kupanua fursa za kujifunza kwa makumi ya maelfu ya watoto na vijana waliokimbia makazi yao.
Baada ya kutangazwa kuwa ndiye mshini Mire mwenye umri wa miaka 36 amesema “Ushidi huu sio wangu peke yangu ni wa watu wote wanaojitolea ninaofanyanao kazi, ni kwa ajili ya watoto walio mashuleni”
Tuzo ya Wakimbizi ya UNHCR ya Nansen iliyoanzishwa mwaka wa 1954 inawaenzi watu binafsi, makundi na mashirika ambayo yanavuka mipaka ya wajibu wa kuwalinda wakimbizi, wakimbizi wa ndani na na watu wasio na utaifa.