Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS imelaani kitendo cha wanajeshi wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel cha kuwalazimisha kuvua nguo Wapalestina wapatao 100 waliowakamata; na kuwakashifu kwa kuwaweka hadharani katika barabara za Ukanda wa Gaza wakiwa wamebaki na nguo za ndani tu.
Sehemu moja ya taarifa hiyo imesema: “kuwavua nguo zao kwa namna ya kuwadhalilisha ni jinai ya wazi ya Wazayuni ya kulipiza kisasi kwa raia wetu wasio na ulinzi kutokana na vipigo wanavyopata askari na maafisa wake kwa wapiganaji wa Muqawama wa Palestina”.
Wataalamu wa sheria wanasema, kuwatendea namna hiyo watu waliokamatwa ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa.
Mamia ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza unaozingirwa na Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu wametiwa nguvuni na kuwekwa kizuizini tangu Hamas ilipoanzisha operesheni ya kushtukiza ya Kimbunga cha Al-Aqsa mnamo Oktoba 7 ili kukabiliana na ukatili wa miongo kadhaa wa utawala dhalimu wa Kizayuni wa Israel.
Tangu wakati huo hadi sasa, jeshi la Kizayuni limeshawaua shahidi zaidi ya watu 17,400 huko Gaza wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto.