Paris Jumanne ya jana ilitangaza kufunga ubalozi wake huko Niamey, mji mkuu wa Niger, na hivyo kuthibitisha mipango iliyoripotiwa hapo awali, baada ya uhusiano kati ya nchi hizo mbili kuzorota kufuatia mapinduzi ya kijeshi katika nchi hiyo ya Kiafrika mwezi Julai 2023.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa amesema katika taarifa: Kwa muda wa miezi mitano, ubalozi wetu umekumbwa na vikwazo ambavyo vimezuia ujumbe wake wa kidiplomasia kutekeleza vizuri majukumu yake nchini Niger.
Taarifa hiyo imeendelea kusema: ‘Vizuizi karibu na ubalozi, kubanwa safari za wafanyakazi na kutoruhusiwa wanadiplomasia kuingia Niger ni ukiukaji wa wazi wa Mkataba wa Vienna wa Mahusiano ya Kidiplomasia.’
Hatua nadra sana ya kufungwa ubalozi huo imechukuliwa kufuatia kuondoka nchini Niger kikosi cha mwisho cha wanajeshi wa Ufaransa mnamo Desemba 22.
Paris na Niamey zimekuwa na uhusiano mbaya kufuatia mapinduzi ya kijeshi mwezi Julai, ambayo yalimuondoa madarakani Rais Mohamed Bazoum, jambo lililochukuliwa kuwa pigo jingine kubwa kwa satwa ya Ufaransa katika eneo hilo baada ya mapinduzi ya kijeshi ya Mali mwaka 2020 na Burkina Faso mwaka 2022.
Kufuatia mapinduzi ya Julai 26, jeshi la Niger lilitaka kuondoka haraka wanajeshi 1,500 wa Ufaransa waliotumwa huko kupambana na Makundi ya kigaidi katika eneo hilo kutokana na kukiukwa mikataba kadhaa ya kijeshi iliyotiwa saini na Paris.
Mwishoni mwa Agosti, utawala wa kijeshi pia uliamuru kufukuzwa balozi wa Ufaransa Sylvain Itté ambaye alikuwa amenaswa ndani ya ubalozi huo kwa karibu mwezi mmoja kabla ya kuondoka.
Shughuli za ubalozi huo sasa zitafanyika kutokea Paris, ambapo Ufaransa itaendelea kuwa na mahusiano na raia wake katika eneo na kusaidia mashirika ya kibinadamu NGOs nchini Niger.
Taarifa iliyotolewa na serikali ya Paris imesema: Tutadumisha uhusiano na raia wa Ufaransa mashinani, na mashirika yasiyo ya kiserikali yanayofanya kazi katika sekta ya masuala ya kibinadamu kwa manufaa ya moja kwa moja ya watu wanaokabiliwa na hatari mbalimbali.’