Maelfu waandamana Ghana kulaani mauaji ya kimbari ya Israel katika Ukanda wa Gaza

Ripoti kutoka Ghana zinasema, maelfu ya raia walijitokeza katika mitaa ya mji wa Kumasi katika maandamano ya kuunga mkono Palestina nchini humo ambapo sambamba na kutangaza mshikamano wao na watu wa Gaza wamelaani pia mauaji ya kimbari ya utawala bandia wa Israel.

Vijana wa kiume na wa kike wakiwemo watoto katika mji wa Kumasi wafuasi wa Palestina, wakiwa wamebeba mabango, maberamu na bendera, walitoa nara za kuunga mkono Palestina na kutoa mwito wa kukomeshwa mara moja mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina huko Gaza.

Baadhi ya mabango ya waandamanaji hao yalisomeka: ‘Acha mauaji ya kimbari’, na ‘kushambulia watoto kwa mabomu si kujilinda”. Maandamano hayo ni sehemu ya “siku ya kimataifa ya hatua kwa Palestina na kutoa wito wa kukomesha umwagaji damu ambao umeua karibu Wapalestina 24,000 na kujeruhi maelfu ya wengine huko Gaza.

Ibrahim Mussa, mwanachama wa wanasoshalisti wa Ghana ambaye alikuwa mmoja wa washiriki wa maandamano hayo ametoa wito kwa asasi za kimataifa hususan Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Araba League) kuisusia Israel pamoja na bidhaa zake.

Aidha balozi wa Palestina nchini Ghana Abdulfatah Ahmed amesema maandamano haya yanalenga kuwaelimisha watu sio tu kuhusu ukatili unaotokea Gaza bali pia historia ya uvamizi huo.

Maelfu ya watu waliokusanyika katikati mwa mji wa Kumasi wakiwemo wanachama wa Harakati ya Vijana wa Palestina waliohudhuria maandamano hayo, wamesema, waandamanaji wana hasira juu ya dhulma inayofanywa huko Gaza dhidi ya Wapalestina wasio na hatia.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *