Afrika Kusini imemvua David Teeger majukumu yake kama nahodha wa Kombe la Dunia lijalo la Kriketi kufuatia matamshi yake ya kuunga mkono jinai za utawala haramu wa Israel.
Siku ya Ijumaa, Shirikisho la Kriketi ya Afrika Kusini (CSA) ilitangaza uamuzi wa kumshusha cheo Teeger kama Nahodha wa timu ya Afrika Kusini ya chini ya umri wa miaka 19 kwa ajili ya hatua za usalama na usalama baada ya hotuba yake katika tuzo za Jewish Achiever Awards.
Teeger alitazamiwa kuiongoza Afrika Kusini katika mashindano ya Kombe la Dunia ya Kriketi ya Vijana wasiozidi umri wa miaka 19, yatakayoanza Januari 19.
CSA ilisema kwenye taarifa kwamba katika hali zote, imeamua David aondolewe unahodha wa mashindano hayo. “Hili ni kwa manufaa ya wachezaji wote, timu na David mwenyewe,” imesema taarifa hiyo.
Teeger aliripotiwa kusema kwamba tuzo aliyopokea mnamo Oktoba ataitunuku jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel
Makundi kadhaa yalikuwa yamewasilisha malalamiko juu ya maoni ya Teeger na baada ya hapo alikuwa chini ya uchunguzi.
Shirikisho la kriketi la Afrika Kusini lilisema kulikuwa na wasiwasi kwamba unahodha wa Teeger unaweza kusababisha mvutano wakati wa mashindano.
Mnamo Januari 4, waandamanaji wanaounga mkono Palestina waliandamana nje ya lango kuu la Newlands mjini Cape Town kabla ya mechi ya majaribio ya Mwaka Mpya kati ya Afrika Kusini na India wakilaani uteuzi wa Teeger.
Kuondolewa kwa Teeger kunakuja wakati Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) ikisikiliza kesi ya Afrika Kusini dhidi ya Israel ya kufanya mauaji ya kimbari huko Gaza.
Afrika Kusini ilichukua nafasi ya Sri Lanka kama wenyeji wa Kombe la Dunia la Wanaume chini ya miaka 19. Sri Lanka ilibadilishwa kutokana na kuingiliwa na serikali katika uendeshaji wa mchezo huo.