Gazeti la Wall Street Journal la Marekani limeripoti kuwa, asilimia 80 ya njia za chini kwa chini za Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS katika Ukanda wa Gaza zingali zinafanya kazi, licha ya mashambulizi ya kinyama ya utawala wa Kizayuni dhidi ya eneo hilo lililozingirwa, tokea Oktoba 7, 2023.
Ripoti ya Wall Street Journal imenukuu maafisa wa Marekani na Israel ambao wamekiri kuwa, asilimia 80 ya handaki hizo zinazotumiwa na HAMAS zingali salama, na kwamba hujuma za mabomu na makombora ya utawala haramu wa Israel katika muda wa siku 114 zilizopita zimeshindwa kuziharibu na kuzisambaratisha.
Kwa mujibu wa ripoti ya jana Jumamosi ya gazeti hilo la Marekani, jitihada za Israel za kubomoa kilomita 482.8 za mtandao wa njia hizo za chini kwa chini za HAMAS katika Ukanda wa Gaza ili kuzuia mashambulizi ya ulipizaji kisasi ya kundi hilo la muqawama hazijafua dafu mpaka sasa.
Gazeti la Wall Street Journal la Marekani limesema Israel haijaambulia chochote licha ya kutumia mbinu mbalimbali kama kumimina maji ya bahari ya Mediterrania kwenye njia hizo za chini ya ardhi katika Ukanda wa Gaza, kutumia maroboti na hata mbwa wa kunusa.
Huko nyuma pia, idara ya usalama wa ndani ya utawala haramu wa Kizayuni wa Israel (Shin Bet) ilikiri juu ya uwezo mkubwa wa njia za chini ya ardhi zilizoundwa na Harakati ya Muqawama ya Palestina HAMAS katika maeneo yote ya Ukanda wa Gaza.
Utawala huo pandikizi umeendelea kuwashambuliwa Wapalestina wa Gaza kwa mabomu, makombora na kila aina ya silaha. Idadi ya vifo vya Wapalestina kutokana na vita vya mauaji ya kimbari vinavyoendelezwa na jeshi katili la Israel huko Gaza tangu Oktoba 7 imepindukia 26,200, na idadi ya waliojeruhiwa ni zaidi ya 64,110.
Aidha taarifa zinasema mashambulizi ya Israel yamesababisha Gaza kuwa eneo lililojaa magofu, huku 60% ya miundombinu ya eneo hilo ikiharibiwa na karibu wakaazi milioni 2 wamelazimika kuyahama makazi yao mbali na eneo hilo kushuhudia uhaba mkubwa wa chakula, maji safi na dawa.