The Intercept: Uhalifu wa kivita unaruhusiwa kwa Israel, ni haramu kwa Sudan

Makala iliyochapishwa kwenye tovuti ya habari ya Marekani, The Intercept, imekosoa misimamo ya kindumakuwili na ya kinafiki iliyochukuliwa na Marekani kuhusu mizozo ya kimataifa, ambayo ilidhihirika wazi katika kushughulikia uvamizi wa Israel kwenye Ukanda wa Gaza, na vita vinavyoendelea nchini Sudan kati ya jeshi rasmi na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF).

Makala hiyo imesema kuwa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imeeleza hatua za Vikosi vya Msaada wa Haraka na makundi yenye silaha yanayoshirikiana navyo kuwa ni “mauaji ya kikabila” na “uhalifu dhidi ya ubinadamu,” lakini imehepa kutoa hukumu juu ya mauaji ya Israel katika Ukanda wa Gaza.

Kwa mujibu wa tovuti hiyo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani inajizuia kufanya uamuzi kama huo wa kuilaani Israel kutokana na mauaji yake dhidi ya maelfu ya watu wa Palestina, badala yake, inatambua hatua za jeshi la Israel na kauli za baadhi ya mawaziri wa utawala huo kuwa haziwakilishi msimamo rasmi wa Tel Aviv.

The Intercept imeandika kuwa, Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani, Antony Blinken amesisitiza kuwa RSF na vikosi vya Jeshi la Sudan vina hatia ya kufanya uhalifu, na tarehe 6 Desemba, alidai kuwa pande zote mbili zilifanya jinai za kivita.

Hata hivyo, wanasema waandishi wa The Intercept, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imekataa kutoa uamuzi kama huo kuhusu vita vya Israel dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza.

Mkurugenzi wa Ofisi ya Human Rights Watch mjini Washington ameiambia tovuti ya The Intercept kwamba maofisa wa serikali ya Marekani wanalaani mara kwa mara vitendo vya pande nyingine zinazopigana katika maeneo kama Ukraine, Ethiopia na Sudan, “lakini linapokuja suala la Gaza, wanaepuka kutoa hukumu juu ya mienendo ya Israel.”

The Intercept imeripoti kuwa, waandishi wa habari humuuliza maswali karibu kila siku msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje Marekani kuhusu ukatili unaofanywa na wanajeshi wa Israel ambao wamewalenga raia katika kanisa moja huko Gaza, kushambulia hospitali, shule, na makazi ya raia kwa mabomu na makombora; Au kuwanyima chakula, mafuta na dawa wakazi wa ukanda huo. Hata hivyo Marekani imekuwa ikijiepusha kuiwajibisha Israel na badala yake inaendelea kuikingia kifua na kuhalalisha mauaji yake ya kimbari huko Gaza.

The Intercept imeripoti kuwa, jumla ya misaada iliyotolewa na Marekani kwa Israel katika kipindi hiki cha vita na mashambulizi ya utawala huo huko Gaza imefikia dola bilioni 158 na kwamba kiwango hicho ni kikubwa zaidi kuliko msaada uliotolewa na Marekani kwa nchi nyingine yoyote tangu baada ya Vita vya Pili vya Dunia.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *