Maelfu ya Wamorocco wamejitokeza tena kwenye barabara za mji mkuu wao Rabat kutoa wito wa kusitishwa uhusiano wa nchi yao na utawala wa Kizayuni wa Israel, ambao wameulaani na kuutaja kuwa kuwa ni mfanya “mauaji ya kimbari” katika Ukanda wa Gaza.
“Kuanzisha uhusiano wa kawaida ni uhaini,” na “Komesheni mauaji ya halaiki,” yamesomeka mabango yaliyobebwa na waandamanaji hadi mbele ya bunge la Morocco katikati mwa mji mkuu Rabat.
Idadi hiyo imelingana na ya maandamano kama hayo yaliyofanyika Novemba katika mji mkuu wa kibiashara wa Morocco Casablanca.
“Tunaona mashambulio ya makombora kwa saa 24 kila siku, watoto wakiuawa, karibu watu 30,000 wamekufa na hakuna kinachozuia mauaji. Mauaji ya kimbari yanaendelea,” amesema Abdelhakim Ziani, mwanafunzi wa udaktari mwenye umri wa miaka 25 ambaye amejiunga na maandamano ya Rabat akitaka kusimamishwa uhusiano kati ya Morocco na utawala haramu wa Israel.
“Hatuwezi kuendelea kuuza na kununua kutoka kwa watu hawa wanaofanya mauaji ya kimbari,”amesisitiza raia huyo wa Morocco.
Maandamano hayo ya Rabbat yameandaliwa na makundi mbali mbali yenye mielekeo ya kisiasa ya mrengo wa kulia na mrengo wa kushoto.
Serikali ya Morocco imeshutumu rasmi kile ilichokiita “ukiukaji wa wazi wa vifungu vya sheria za kimataifa” uliofanywa na Israel katika vita vyake dhidi ya Gaza lakini haijaonyesha ishara yoyote ya kubadilisha msimamo iliochukua wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel ambao umelaaniwa na kukosolewa vikali katika Ulimwengu wa Kiislamu…/