Mvutano wa kidiplomasia kati ya Misri na utawala wa Kizayuni wa Israel umeongezeka kufuatia matamshi yenye utata yaliyotolewa na waziri wa Israel ya kuihusisha Cairo na matukio ya Oktoba 7.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri imetoa taarifa ya kulaani ilichokiita matamshi ya “kuaibisha” na “ya kutowajibika” ya waziri wa fedha wa mrengo wa kulia wa wa utawala wa Kizayuni Bezalel Smotrich ambaye amedai, Cairo “ina dhima kubwa” kwa shambulio la Hamas la Oktoba 7.
Kwa mujibu wa shirika la umma la utangazaji la Israel, Kan, Smotrich amesema wakati wa mkutano wa chama chake cha Religious Zionism kwamba “Wamisri wanabeba dhima kubwa kwa Oktoba 7”.
Waziri huyo wa utawala wa Kizayuni amedai kuwa “silaha nyingi za Hamas zinapitia Misri”, ambayo ina mpaka wa pamoja na Gaza na imekuwa mpatanishi mkuu katika juhudi za kukomesha mapigano.
Akijibu tuhuma hizo, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri Ahmed Abu Zeid amesema “inasikitisha na inaaibisha” kwa waziri wa Israel “kuendelea kutoa matamshi ya kutowajibika na ya uchochezi”.
Abu Zeid amesema, Misri inadhibiti kikamilifu eneo lake, na hairuhusu upande wowote ule ulihusishe jina la Misri katika majaribio yaliyoshindwa ya kuhalalisha mapungufu yake.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje amebainisha kuwa, matamshi ya Smotrich yanaakisi “njaa kali ya mauaji na uharibifu na hujuma dhidi ya jaribio lolote la kuudhibiti mgogoro wa Ukanda wa Gaza”.
Wakati huohuo, mtandao wa Habari wa Al-Qahera wa Misri umetangaza kuwa Cairo “inafuatilia kwa karibu hali ya mambo” huko Rafah, na “imeshajiweka tayari kukabiliana na kila hali”.
Mashambulizi ya kinyama yanayoendelea kufanywa na utawala haramu wa Israel yamesukuma zaidi ya nusu ya watu wote milioni mbili na laki nne wa Gaza iliyozingirwa kwenye eneo la kubwa la mahema katika mji wa kusini wa Rafah kwenye mpaka wa pamoja na Misri.
Israel imeanza kuiangazia Rafah kama eneo jipya la Gaza la kuliandama kwa mashambulio yake ya kinyama huku wasiwasi ukizidi kuongezeka wa jeshi la utawala huo kuanzisha uvamizi wa nchi kavu dhidi ya eneo hilo…