Yoav Gallant, Waziri wa Vita wa utawala wa kibaguzi wa Israel amekiri kuhusu hasara kubwa liliyopata jeshi la utawala huo katika vita vya Gaza na kusema, Wazayuni hawajawahi kukabiliwa na vita kama hivyo kwa muda wa miaka 75 iliyopita.
Siku ya Jumatano, Waziri wa Vita wa utawala wa Kizayuni alikiri kuhusu hasara kubwa ya jeshi la utawala huo katika vita vya Gaza na kusema hasara hiyo ya vifo, majeruhi na kifedha ilikuwa haijawahi kushuhudiwa tena tangu kuasisiwa utawala huo haramu. Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari vya Israel, tangu kuanza vita vya Gaza, takriban wanajeshi 560 wa Kizayuni wameuawa na wengine takriban 3,000 wamejeruhiwa katika mapigano huko Gaza. Idadi hiyo ya wanajeshi wa Kizayuni waliouawa na kujeruhiwa katika vita na wapiganaji wa muqawama wa Palestina huko Gaza, inaripotiwa katika hali ambayo jumla ya askari wa utawala huo waliouawa katika vita vyake viwili na nchi za Kiarabu katika miaka ya 1967 na 1973 walikuwa takriban 700 na 2500 mtawalia.
Mbali na hasara kubwa ya askari wa Israel katika vita vya Gaza, duru za Kizayuni zinakiri kuwa katika vita hivyo vya miezi 5, muundo wa kiuchumi wa utawala huo pia umepata hasara kubwa ya dola bilioni 50. Yoav Gallant, amekiri hali ngumu ya Israel dhidi ya muqawama wa makundi ya Wapalestina huko Gaza na kuongeza kuwa Tel Aviv inalazimika kufanyia marekebisho sheria ya huduma za kijeshi na kuziba pengo lililoachwa wazi na askari waliouawa na kujeruhiwa ili kuweza kuendeleza vita. Kukiri kwa afisa huyo mkuu wa kijeshi wa Israel kuhusu kushindwa kukabiliana na muqawama wa Palestina kunafanyika katika hali ambayo katika historia yake ya miaka 75, utawala huo umekuwa ukichukulia nguvu za kijeshi na makabiliano ya haraka na Waarabu, kuwa nukta za nguvu na ubora za utawala huo wa kigaidi.
Vita vya Gaza, licha ya hasara kubwa ya kibinadamu kwa raia wa Palestina, ambayo jamii ya kimataifa inaitaja kuwa mauaji ya kimbari ambayo yalikuwa hayajawahi kushuhudiwa tena katika karne ya 21, mbali na kulisababishia maafa na hasara kubwa jeshi la Israel pia vimeusababishia utawala huo hasara kubwa za kiuchumi na wakati huo kuibua changamoto katika muundo wa kisiasa wa utawala huo katika wiki za karibuni. Katika uwanja huo, mvutano mkali umeibuka katika Baraza la Mawaziri la Vita kwa kadiri kwamba ni nadra kuwaona Benjamin Netanyahu, waziri mkuu na Benny Gantz, mjumbe katika baraza hilo wakizungumza ana kwa ana.
Vyombo vya habari vya Kizayuni vimeripoti katika siku za karibuni kwamba wakati Benjamin Netanyahu amekataa pendekezo la Mossad na Shabak (mashirika ya ujasusi na usalama wa ndani) la kufanya makubaliano na Hamas, Gadi Eisenkot, mjumbe mwingine wa baraza hilo, amesema uamuzi wa Netanyahu kuhusu timu ya kufanya mazungumzo ya kubadilishana mateka na Hamas, si wa kimantiki na kuwa unaongeza tu hitilafu katika baraza la mawaziri.
Ishaq Brik, jenerali wa jeshi la Kizayuni anasema kuhusiana na kushindwa utawala huo ghasibu kukabiliana na makundi ya muqawama ya Palestina na matokeo mabaya ya kuendelea vita huko Gaza kuwa iwapo majeshi ya Israel yataingia katika mji wa mpakani wa Rafah, ambao una wakimbizi wapatao milioni moja na nusu wa Kipalestina, si tu hayatafanikiwa kufikia lengo la kuiangamiza Hamas, bali yatajiweka katika hali ngumu zaidi ya kiusalama na kupata hasara zaidi. Jenerali huyo wa Israel ameongeza kuwa, vita vya Gaza vimewatenga Wazayuni na jumuiya ya kimataifa na kuwa kuendelea kwake bila shaka kutaitumbukiza Israel katika kina kirefu cha misukosuko ya kiuchumi, kiusalama, kijamii na hatimaye kuharibu uhusiano wake wa kigeni na mataifa mengine.
Juhudi za maafisa wakuu wa utawala wa Kizayuni za kuendeleza vita na kupinga usitishaji mapigano ni kinyume na mtazamo wa jumuiya ya kimataifa, huku Wazayuni wengi pia wakiamini kuwa utawala huo, baada ya kupita takriban miezi 5 ya hujuma kali ya kijeshi katika Ukanda wa Gaza, haujafanikiwa lolote zaidi ya kufanya mauaji ya kimbari dhidi ya raia, na kuwa sasa umenasa kwenye kinamasi cha ukanda huo. Ni kwa kuzingatia hilo ndipo baadhi ya wachambuzi wa mambo wakaamini kuwa mienendo ya Netanyahu kuhusu suala hilo inathibitisha wazi kuwa anataka kukwepa lawama na kufunika kushindwa jeshi la Israel pamoja na juhudi zake za kidiplomasia kuhusu vita vya Gaza na uwezekano wa kuvunjwa baraza lake la mawaziri baada ya kumalizika vita. Maoni mengi kuhusu kukata tamaa Benjamin Netanyahu na kushindwa jeshi la Israel dhidi ya wapiganaji wa muqawama yanatolewa katika hali ambayo utawala ghasibu wa Kizayuni ulianzisha mauaji makubwa katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan dhidi ya wananchi wasio na ulinzi na madhulumu wa Palestina tangu Oktoba tarehe 7, 2023, kwa uungaji mkono kamili wa nchi za Magharibi. La kusikitisha zaidi ni kwamba mauaji hayo dhidi ya watoto na wanawake wa Kipalestina yanaendelea katika hali ambayo jumuiya ya kimataifa na taasisi za haki za binadamu zimenyamazia kimya jinai hizo za kutisha za Israel dhidi ya jamii ya mwanadamu.