Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amewataka majenerali wa kijeshi nchini Sudan waheshimu mwezi mtukufu wa Ramadhani na ametoa mwito wa kusitishwa mapigano wakati wa mwezi huo mtukufu.
Akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Guterres amesema: “Ninatoa mwito kwa pande zote nchini Sudan kusitisha vita na kuheshimu maadili ya mwezi mtukufu wa Ramadhani. Usitishaji vita huo lazima upelekee kuwekwa chini silaha kikamilifu na kuandaliwa mazingira thabiti ya kupatikana amani ya kudumu kwa wananchi wa Sudan.” Ameongeza kuwa: “Lazima maadili ya Ramadhani yaheshimiwe kikamilifu.”
Siku chache zijazo Waislamu kote ulimwengu wataingia kwenye mwezi mtukufu wa Ramadhani, mwezi wa toba na kurekebisha makosa waliyofanya, mwezi wa kuhurumiana na ni mwezi wa kujipinda kwa ibada.
Kikao hicho cha Baraza la Usalama kuhusu Sudan kimefanyika kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani, Machi 7, 2024.
Tarehe 15 mwezi ujao wa Aprili, mgogoro wa vita vya kuwania madaraka baina ya majenerali wa kijeshi nchini Sudan utatimiza mwaka mmoja huku mapigano ya kikatili kati ya Jeshi la Sudan na Vikosi vya Msaada wa Haraka yakiendelea bila ya kuweko matumaini ya kutatuliwa mgogoro huo.
Vita hivyo vya uchu wa madaraka vimesababsiha madhara makubwa kwa watu wa Sudan na miundombinu ya nchi hiyo na hivi sasa vimezidi kuhatarisha umoja wa ardhi ya Sudan.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameonya kwa kusema kwamba, kuna hatari kubwa ya mgogoro huo kuchochea ukosefu wa utulivu wa kikanda katika eneo zima la kutokea Sahel hadi Pembe ya Afrika na Bahari ya Shamu au Bahari Nyekundu.