Hatua ya Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania ya kumteua aliyekuwa Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Paul Makonda kuwa mkuu wa mkoa wa Arusha imezusha gumzo na mitazamo kinzani baina ya wachambuzii na wananchi wa Tanzania kwa ujumla.
Rais Samia Suluhu Hassan jana Jumapili alifanya mabadiliko ya viongozi mbalimbali katika serikali yake, wakiwemo mawaziri, naibu mawaziri, makatibu wakuu, wakuu wa mikoa na wilaya.
Hata hivyo uteuzi uliogusa wengi ni ule wa Paul Makonda kuwa mkuu wa mkoa wa Arusha, mizi michache tu baada ya kuteuliwa kuwa Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM. Makonda alikuwa amehudumu katika nafasi yake ya awali kwa karibu miezi mitano.
Baadhi ya wachambuzi wa siasa za Tanzania wanauliza je, kuondolewa Makonda katika nafasi ya Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM na kufanywa mkuu wa mkoa wa Arusha ni kumshusha cheo au kumpandisha?
Wakili wa kujitegemea, Peter Madeleka amekosoa utendaji wa Paul Makonda wakati alipokuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM hasa mienendo yake ya kutoa maagizo na kwa mawaziri wa serikali na kuandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa X kwamba: Makonda hakuwa na mamlaka yoyote ya kutoa maagizo kwa mawaziri.
“Naona wajibu wa kumfundisha Makonda somo la Katiba na sheria hasa kuhusu haki za binadamu…”, amesema Madeleka kwenye mtandao wa X.
Gazeti la Mwananchi la Tanzania limemnukuu kada wa chama cha upinzani Chadema, Mdude Nyangali akisema: “Makonda aliteuliwa kuwa mwenezi siku ya hukumu ya kesi ya bandari ya Dar es Salaam kwa lengo la kuhamisha agenda ya hukumu ya bandari lakini kwa bahati mbaya agenda haikuhama…”.
Baada ya kuteuliwa kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Paul Makonda alikuwa mwiba mkali kwa mawaziri na watendaji wa serikali na alikuwa akikosolewa sana kwa kuingilia mambo yaliyo nje ya mamlaka yake ikiwa ni pamoja na kesi za mahakama.
Baadhi ya wachambuzi pia wanasema mabadiliko yaliyofanywa na Rais Samia wa Tanzania yumkini yakawa ya kimkakati kwa ajili ya kupata ufanisi zaidi katika maeneo husika wakati huu nchi hiyo inapoelekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu mwaka 2025.