Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika (AUPSC) limetoa mwito wa kupewa ufadhili wa kutosha, endelevu na wa kuaminika kwa ajili ya kufikia malengo yake ya mwaka 2025 baada ya kuondoka Ujumbe wa Mpito wa AU nchini Somalia (ATMIS) mwezi Desemba mwaka huu.
Taarifa ya baraza hilo imesema: “AUPSC inakaribisha pendekezo la serikali ya Somalia kuhusu hali ya kulinda usalama itakavyokuwa baada ya kuondoka askari wa ATMIS nchini humo na inazingatia ombi la Somalia la kuitaka AU iendelee kuwepo nchini humo kuisaidia serikali hiyo kila itakapohitajika.”
Kikosi cha ATMIS kinatazamiwa kuondoka Somalia mwezi Desemba mwaka huu. Lakini maandalizi yanaendelea kufanywa ili kuruhusu kupelekwa timu nyingine ya AU ya kusaidia kulinda mafanikio yaliyopatikana hadi hivi na kuhakikisha kuwa Somalia hairejei tena katika hali mbaya ya ukosefu wa usalama iliyokuwa nayo kabla ya AU kupeleka wanajeshi wake nchini humo.
Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika (AUPSC), ambacho ni chombo cha kuchukua maamuzi cha AU kwa ajili ya kuzuia, kusimamia na kutatua migogoro, limesisitizia haja ya kuendelea kuisaidia Somalia na kuendelea kutoa mafunzo kwa vikosi vya usalama vya nchi hiyo ambayo hadi hivi sasa bado inaendelea kupambana na magaidi wa al Shabab.
Hadi hivi sasa ATMIS imeshaondoa wanajeshi 5,000 nchini Somalia na kukabidhi kambi 13 za kijeshi kwa Vikosi vya Usalama vya Somalia wakati wa awamu ya kwanza na ya pili ya zoezi la kupuunguza askari wake nchini humo liliomalizika mwaka 2023.
Timu hiyo ya Umoja wa Afrika ambayo inaonekana imefanikiwa katika kazi zake nchini Somalia, inajiandaa kuondoa wanajeshi 4,000 waliobakia nchini humo mwezi Juni mwaka huu na kukabidhi mambo yote mikononi mwa serikali ya Mogadishu.