Afisa wa jeshi la Iraq amesema kuwa kundi la kigaidi la Daesh (ISIS) bado lina wapiganaji 400 hadi 500 katika nchi hiyo.
Qais Al-Mohammadawi, Naibu wa Kamandi ya Operesheni ya Pamoja, ambayo inasimamia ushirikiano wa vikosi vya usalama vya Iraqi na muungano wa kimataifa, ametangaza kuwa wapiganaji wa kundi la kigaidi la ISIS nchini Iraq ni baina ya 400 na 500 na wapo katika mikoa mitatu hadi minne ya Iraq. Amesema Daesh haina tena uwezo wa kusajili wapiganaji wapya.
Al-Mohammadawi ameongeza kuwa, wapiganaji hao wa Daesh wanafanya mashambulizi ya hapa na pale dhidi ya vikosi vya usalama na raia wa Iraq.
Ameongeza kuwa kulingana na makadirio ya ripoti ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa , ISIS ina wanachama na wafuasi kati ya 5,000 na 7,000 katika nchi za Iraq na Syria, na nusu yao ni wapiganaji.
Vikosi vya jeshi la Iraq na harakati ya al Hashd al-Shaabi zinaendelea kusaka na kufuatilia na kumaliza kabia mabaki ya Daesh kote nchini Iraq ili kuhakikisha kuwa ISIS na wawapiganaji wake hawajitokezi tena.