Afisa wa zamani wa kikosi cha mauaji wakati wa utawala wa Jammeh atiwa nguvuni Gambia

Jeshi la Gambia limemtia mbaroni kamanda wa zamani ambaye alidaiwa kuwa mwanachama wa ‘kikosi cha mauaji” wakati wa utawala wa rais wa zamani wa nchi hiyo, Yahya Jammeh.

Brigedia Jenerali Bora Colley anadaiwa kuwa alikuwa kiongozi wa kikosi cha wanamgambo kilichopewa jina la utani la “Junglers” ambacho kwa muda mrefu kilikuwa kimetuhumiwa na Umoja wa Mataifa na mashirika ya kutetea haki za binadamu kwa kutekeleza mauaji na utesaji huko Gambia.

Brigedia Jenerali Colle alikamatwa juzi usiku Agosti 9 wakati alipojisalimisha mwenyewe kwa polisi katika kambi ya Yandum. Idara za intelijinsia za Gambia zilifanya oparesheni za uchunguzi karibu na makazi yake katika mji mkuu, Banjul, siku hiyo alipotiwa mbaroni.

Bora Colley bado anashikiliwa na anaendelea kushirikiana na jeshi la polisi katika uchunguzi.

Serikali ya Gambia mwaka 2022 iliidhinisha mapendekezo ya tume iliyochunguza ukatili uliofanywa  wakati wa uongozi wa Rais Yahya Jammeh, huku vyombo vya mahakama vikiafiki kuwafungulia mashtaka watu 70, akiwemo rais wa zamani aliyeingia madarakani katika  mapinduzi ya mwaka 1994.

Jammeh, ambaye utawala wake wa miaka 22 katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi uliandamana na madai mengi ya ukiukaji wa haki za binadamu, alishindwa katika uchaguzi wa rais mwezi Disemba 2016 na aliyekuwa kiongozi wa upinzani Adama Barrow.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *