AFRICA CDC: Mlipuko wa Ebola Uganda umedhibitiwa, unakaribia kumalizika

Mlipuko wa Ebola nchini Uganda umedhibitiwa na unaweza kutangazwa kuwa umekwisha katika siku chache zijazo, kwani zimepita siku 39 tangu kisa cha mwisho cha virusi hivyo kuripotiwa. Hayo ni kwa mujibu wa tangazo la Vituo vya Afrika vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (AFRICA CDC).

Ahmed Ogwell Ouma, kaimu mkuu wa AFRICA CDC amesema hadi kufikia Ijumaa zilikuwa zimepita siku 39 tangu kuthibitishwa kesi ya mwisho na hivyo Ikiwa hakuna kesi mpya zilizoripotiwa ifikapo Januari 10, mlipuko huo utakuwa umekwisha.

Alikuwa akizungumzia miongozo ya Shirika la Afya Duniani (WHO), ambapo nchi inahitaji kusubiri siku 42 ili kuhakikisha kuwa Ebola imetokomezwa.

Pia aliipongeza serikali ya Uganda kwa jinsi ilivyochukua hatua bora za kuzuia kuenea kwa virusi hivyo, akisema ilichukua takriban siku 70 kudhibiti hali hiyo.

Mkurugenzi mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus, katika mkutano wa hivi majuzi na wanahabari tarehe 4 Januari alitaja jinsi mlipuko wa Ebola nchini Uganda ulivyokuwa ukiendelea na kusema kwamba  kuna “habari njema.”

Katika habari nyingine njema, Ebola nchini Uganda haijagunduliwa tangu tarehe 27 Novemba. Ikiwa hali hii itaendelea  na hakutakuwa na kesi ifikapo Januari 11, mlipuko huo utatangazwa kuwa umeisha,” amesema.

Mlipuko wa hivi karibuni wa Ebola nchini Uganda ulitangazwa tarehe 20 Septemba. Ebola iliyozuka nchini humo ni aina ya Sudan, ambayo ni nadra sana barani Afrika kuliko ile ya Zaire. Hii ni mara ya kwanza katika zaidi ya muongo mmoja ambapo Uganda iliripoti mlipuko wa virusi vya Ebola aina ya Sudan.

Kufikia sasa, kulingana na WHO, nchini Uganda kumekuwa na kesi 142 na vifo 55.

Mapema Desemba, mgonjwa aliyejulikana mwisho aliruhusiwa kutoka hospitali. Katika mwezi huo huo, Rais wa Uganda Yoweri Museveni aliondoa vikwazo vyote vinavyohusiana na Ebola vilivyowekwa ili kukabiliana na mlipuko huo, akionyesha maendeleo katika udhibiti wa ugonjwa huo na kudhibiti kuenea kwake.

WHO hivi majuzi ilisambaza  dozi 1,200 za chanjo dhidi ya Ebola aina ya Sudan nchini Uganda.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *