Afrika Kusini yapinga Israel kujiunga na Umoja wa Afrika

Waziri wa Mambo ya Nje wa wa Afrika Kusini amesema kujiunga utawala wa Kizayuni wa Israel na Umoja wa Afrika ni sawa na tusi kwa moyo wa hati ya umoja huo.

Kwa mujibu wa ripoti ya shirika la habari la IRNA siku ya Jumamosi, Naledi Pandor, Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini alisema, “Tunashuhudia mshikamano mkubwa zaidi na mapambano ya watu wa Palestina nchini Afrika Kusini, na tunafungamana na kujitolea kwa ajili ya Palestina. Tuna yakini kwamba mshikamano huu hauko tu katika nyanja ya umma nchini Afrika Kusini, bali pia katika bara zima la Afrika.”

Afisa huyo wa Afrika Kusini amesisitiza kuwa, kukubaliwa utawala wa Kizayuni kujiunga na Umoja wa Afrika ni ukiukaji wa haki za binadamu na ukiukaji wa Hati ya Umoja wa Afrika kwa sababu utawala wa Israel ni nembo ya matatizo yote  na haustahiki kualikwa kuwa mwanachama mwangalizi katika umoja huo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini ameahidi kuwa nchi yake itajaribu kuuzuia utawala wa Kizayuni kupata hadhi ya mwangalizi au nafasi nyingine yoyote sawa na hiyo katika Umoja wa Afrika.

Ameongeza: Afrika Kusini inaamini kanuni za kibinadamu na inazingatia jibu pekee linalofaa kwa maombi kama hayo ni kutokubaliwa uanachama huo.

Februari mwaka huu, Umoja wa Afrika, katika mkutano wake wa 35 wa kilele mjini Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia, uliahirisha uamuzi ambao hapo awali ulichukuliwa kwa upande mmoja mwezi Juni 2021 na Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki, kuupa utawala haramu wa Israel hadhi ya mwangalizi katika Umoja wa Afrika. Viongozi wa Afrika wanatazamiwa kujadili kadhia hiyo katika kikao chao mwakani.

Utawala wa Kizayuni ulikuwa mwanachama wa Jumuiya ya Nchi Huru za Afrika (OAU) kama mwangalizi, lakini ulipoteza hadhi hiyo baada ya kuvunjwa kwa jumuiya hiyo na kuundwa Umoja wa Afrika (AU) mwaka 2002.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *