Nchi za Jumuiya ya BRICS ya mataifa yanayoibukia kiuchumi inataka kutupilia mbali sarafu ya dola ya Marekani na badala yake kuunda mfumo bora wa malipo ambao hautapendelea nchi tajiri.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini Naledi Pandor katika mahojiano na Shirika la Sputnika la Russia. Kundi la BRICS linazileta pamoja Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini.
Naledi Pandor ameongeza kuwa, “Siku zote tumekuwa na wasiwasi na ukweli kwamba kuna utawala wa dola na kwamba tunahitaji kuangalia njia mbadala … Mifumo iliyopo kwa sasa ina mwelekeo wa kupendelea nchi tajiri na inaelekea kuwa changamoto kwa nchi, kama Afrika Kusini.”
Pandor amesema kuwa moja ya sababu zilizopelekea BRICS kuanzisha Benki ya Maendeleo Mpya (NDB) inayoendeshwa kwa pamoja mwaka 2014 ilikuwa ni kutafuta njia mbadala ya malipo.
Waziri wa Mambo ya Nje Naledi Pandor pia amesema kuwa Afrika Kusini imeionya Marekani kwamba mswada unaotaka kukabiliana na kile kinachodaiwa “shughuli mbovu” za Russia barani Afrika unahitaji kutupiliwa mbali kwa sababu unakiuka sheria za kimataifa.
Waziri huyo amesema, “Ninaamini mswada huo unapaswa kutupiliwa mbali kwa sababu ni uingiliaji unaokwenda kinyume na sheria za kimataifa, na tumeliweka wazi hili kwa Marekani.”
Rasimu ya sheria iliyowasilishwa katika Baraza la Wawakilishi la Kongresi mwezi Aprili na Mwakilishi Gregory Meeks ilipitishwa mnamo Mei mwaka jana na inasubiri kura ya Seneti. Iwapo mswada huo utapitishwa, utamtaka Waziri wa Mambo ya Nje kubuni mkakati wa kukabiliana na ushawishi wa Russia barani Afrika na kuziwajibisha serikali za Afrika zinazoshirikiana na Russia.
Kuhusu suala la vikwazo vya upande mmoja vya Marekani, Pandor amebainisha kuwa nchi yake imeitaka Marekani kuhakikisha kwamba vikwazo vyake vya upande mmoja vinaangaliwa upya kutokana na athari zake hasi kwa nchi zingine.