Afrika Kusini imetangaza maafa ya kitaifa baada ya mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa iliyonyesha hivi karibuni nchini humo kuuwa watu saba. Watu wengine wengi hawajulikani walipo hadi sasa. Haya yameelezwa na Kituo cha Kukabiliana na Majanga katika majimbo kadhaa nchini Afrika Kusini.
Wakati huo huo taarifa kutoka Ofisi ya Rais wa Afrika Kusini imeeleza kuwa, serikali imetangaza maafa ya kitaifa nchini humo ili kuwezesha kuchukuliwa hatua endelevu na za pamoja kwa ajili ya kukabiliana na athari za mafuriko. Hali mbaya ya hewa inaripotiwa kutishia majimbo 7 kati ya 9 ya nchi hiyo, hususan kwenye pwani ya mashariki, eneo ambalo linapakana na Bahari ya Hindi.
Watu 5 wamepoteza maisha katika jimbo la KwaZulu -Natal. Hii ni kwa mujibu wa Bi Nonala Ndlovu msemaji wa Kituo cha Kukabiliana na Majanga katika jimbo la Pwani pale alipozungumza na Shirika la Habari la Ufaransa. Mtoto mmoja mchanga ni kati ya watu waliopoteza maisha kufuatia mafuriko hayo. Kichanga hicho kimepoteza maisha baada ya nyumba yao kujaa maji. Watu wengine kadhaa hadi sasa hawajulikani walipo baada ya kujaribu kuvuka mto uliofurika maji ya mvua.
Huko katika jimbo la Limpopo kaskazini mwa Afrika Kusini, jimbo linalopakana na Zimbabwe, hospitali moja imepata madhara kufuatia mafuriko hayo. Barabara na madaraja nayo hayakusalimika kutokana na mvua kubwa zilizosababisha mafuriko huko Afrika Kusini.
Kituo cha Hali ya Hewa cha nchi hiyo kimetabiri kuendelea kunyesha mvua kubwa mtawalia huku kukiwa na hatari ya kutokea tena mafuriko kutokana na udongo na mito kujaa maji.
Afrika Kusini mwaka jana ilikumbwa na mafuriko makubwa zaidi kuwahi kuiathiri nchi hiyo katika historia. Mafuriko hayo yaliliathiri sana jimbo la Durban ambao ni mji wa tatu kwa ukubwa na wenye bandari kuu barani Afrika. Mvua hiyo kubwa ilisababisha maporomoko ya udongo ambayo yalisomba watu, madaraja, barabara na majengo.
Watu zaidi ya 400 walipoteza maisha na wengine zaidi ya 85,000 walidhurika kwa mafuriko ya mwaka jana nchini Afrika Kusini.