Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini ametetea uamuzi wa nchi yake wa kufanya mazoezi ya pamoja ya jeshi la majini kati yake na nchi kubwa za Russia na China mwezi ujao wa Februari katika pwani yake ya mashariki mwa nchni hiyo ya kusini mwa Afrika.
Afrika Kusini ni mwanachama wa BRICS, kambi ya nchi zinazoinukia kiuchumi. Kambi hiyo inajumuisha nchi za Brazil, Russia, India na China.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini, Bi Naledi Pandor amesema: “Nchi zote zinafanya mazoezi ya kijeshi na marafiki zao kote ulimwenguni. Hivyo kisiwe ni kioja kwa nchi yoyote kufanya mazoezi na washirika wengine. Hiyo ni sehemu ya njia kuu na ya kimsingi ya kuimarisha uhusiano kati ya nchi na nchi.
Amesema mataifa ya Afrika yanapaswa kukataa kuburuzwa na madola yanayosema: “ninachofanya mimi ni sawa, lakini huwezi wewe kufanya hivyo kwa sababu wewe ni nchi inayoendelea, au wewe ni nchi ya Afrika. Hayo ni mazoea ya unyanyasaji kimataifa.”
Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini vile vile amenukuliwa akisisitiza kuwa nchi yake haitaburuzwa katika kuunga mkono upande wowote wa vita vya Ukraine na imezikosoa nchi za Magharibi kwa kuishutumu Russia huku zikipuuza hatua nyingine za uvamizi wa kichokozi kama mashambulizi yanayofanywa kila siku na Wazayuni pamoja na ukaliaji mabavu wa utawala wa Israel katika ardhi za Palestina.
Nchi zote mbili yaani Russia na Afrika Kusini zimekuwa zikishirikiana kibiashara kwa miaka kadhaa sasa huku uuzaji wa bidhaa na mabadilishano ya kibiashara baina ya pande mbili nayo yakisizidi kuongezeka. Kiwango cha bidhaa za Afrika Kusini zinazouzwa nchini Russia kilifikia dola milioni 587 mwaka 2020 huku uuzaji wa bidhaa za Russia nchini Afrika Kusini ukifikia dola milioni 506 katika mwaka huo.