Ajali ilivyopoteza mke, watoto wawili

Dodoma. “Binadamu ni wasafiri, lakini njia za kusafiria zinatofautiana, hata hivyo nimeamua kusahau na kusamehe.” Hiyo ni kauli ya Meshack Samson, aliyepoteza watu watatu katika ajali ya gari iliyohusisha mkokoteni wa kuvutwa na ng’ombe.

Ilikuwa ni umbali wa karibu kilomita 70 kutoka katikati ya Jiji la Dodoma hadi Kijiji cha Manzase wilayani Chamwino, katika barabara ya kuelekea Iringa kulikotokea ajali iliyochukua maisha ya watu saba.

Katika ajali hiyo Meshack alipoteza mke na watoto wawili huku ikichukua maisha ya watu wengine wanne wa familia tofauti.

Samson anaikumbuka Julai 3 mwaka huu, siku itakayobaki kwenye kumbukumbu za maisha yake baada ya kuamshwa alfajiri na mwito wa simu ya mkewe (Helena Makwawa) wakiwa wamelala nyumbani pamoja.

Anasema alishtuka na kumuuliza ni nani aliyekuwa anampigia simu muda huo kwa kuwa si kawaida ya kuwa na mawasiliano nyakati za usiku.

“Alinijibu, huyu ni Jonas, tumemuomba atukodishe mkokoteni kwa ajili ya kuelekea milimani kuchukua udongo kabla ya jua halijachomoza,” anasema Samson alivyojibiwa na mkewe huku akionyesha huzuni.

Anasema baada ya mkewe kuongea na simu hiyo aliamka na kuanza kujiandaa kwa ajili ya kuongozana na Jonas ambaye anamiliki mkokoteni wa kuvutwa na ng’ombe kijijini hapo.

Samson alisema mkewe alikuwa ana mtoto mdogo wa mwaka mmoja na nusu (Irene Samson) waliyeshauriana kwa muda kama amuache au aende naye milimani.

Anasema baada ya mashauriano hayo walikubaliana aende na mtoto kwa kuwa akiamka na kumkosa mama yake angewasumbua.

Kama ni simulizi ungeweza kusema, kifo kilikuwa kinamwita mtoto huyo, kwa kuwa mabishano hayo yalidumu kiasi lakini mwisho ukawa aende naye tu hakuna namna.

Safari ikaanza

Katika msafara huo mkewe aliwachukua watoto wake wengine aliowataja kwa majina ya Anthony Samson (12) na Vaileth Samson (14).

Anasema baada ya kujiandaa walianza safari, huku akimweleza kuwa wanampitia na Mwajuma Chilewa, mkazi wa kijiji hicho ili waungane kwenye msafara huo uliokuwa wa kuungana ili kupunguza gharama za kulipia mkokoteni mmoja mmoja.

Samson, anayejishughulisha na kuuza maji kwenye mkokoteni, aliamka saa 12 asubuhi na kuanza kusambaza maji katika vijiji jirani kabla ya kupokea taarifa yoyote.

Alivyosikia taarifa

Anasema akiwa njiani alipata simu kutoka kwa mmoja wa wanakijiji wenzie wakimtaarifu kuhusu ajali iliyotokea Kijiji cha Lugala ambayo hakuwa na hofu zaidi ya kuhoji ilikuwa ajali ya namna gani.

“(mwanakijiji) akaniuliza umesikia Jonas amepata ajali? Amegongwa na gari, nikashtuka sana nikiwaza Jonas ndiye aliyekuwa na watoto wangu kwenye mkokoteni wake; je, familia yangu itakuwa salama kweli!” alishangaa.

Samson alisema baada ya kupokea taarifa hizo, alianza safari kuelekea barabarani na njiani alikutana na kundi la watu wakielekea sehemu ya tukio akaungana nao.

Alisema baada ya kukaribia eneo la tukio alikuta maiti zimezagaa eneo hilo na macho yaligongana na maiti ya binti yake, Vaileth.

“Watu wakanishika pale na kunisogeza pembeni wakinibembeleza, lakini nikajikaza kama mwanamume na kuanza kuiangalia familia yangu,” anasema huku akijifuta machozi.

“Iliniuma sana kuona mke na mtoto wangu tena wa kunyonya akiwa chini hapumui tena, ndugu zangu maumivu haya sijui wa kunipokea mwenzenu namuachia Mungu.”

Samson anasema baada ya hapo taratibu za kupeleka majeruhi Hospitali ya Mkoa wa Dodoma zilianza, huku miili ya marehemu ikirudishwa nyumbani kwa ajili ya taratibu za mazishi.

Mbali na kurudisha maiti tatu nyumbani, lakini alikuwa na kibarua kingine cha kuwaza kuhusu mtoto wake, Anthony aliyekuwa amekimbizwa hospitali kupatiwa matibabu.

Familia ya Meshack ilikuwa na jumla ya watoto sita, hivyo amebaki na jukumu la kulea watoto wanne ambao sasa hawana mama tena.

Diwani wa Manzase, John Mika anasema miili ya watu saba iliagwa katika Kanisa la Mtakatifu Marco.

Anasema baadhi ya miili ya watu hao saba ilizikwa katika kijiji hicho.

Historia ya eneo hilo

Diwani wa kata hiyo, Mika anasema sehemu iliyotokea ajali hiyo zimekuwa zikitokea mara kwa mara, ikiwamo ya mwaka jana iliyoua watu wawili.

Kiongozi huyo aliomba uongozi wa mkoa kuliangalia eneo hilo kwa kuweka matuta ili kupunguza uwepo wa ajali hizo na kunusuru maisha ya watu.

Chanzo cha ajali

Awali, akizungumzia ajali hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Martin Otieno anasema chanzo cha ajali ni gari la Idara ya Maji Mkoa wa Katavi iliyokuwa inaendeshwa na Paschal Paulo (29) kugonga mkokoteni uliokuwa unakokotwa na ng’ombe ukiwa umebeba watu 12.

Otieno anasema gari hiyo ilikuwa kwenye mwendokasi na kushindwa kuuona mkokoteni huo ndipo aliugonga kwa nyuma na kusababisha kupinduka.

Mbali na vifo vya watu saba, ng’ombe wawili waliokuwa wanavuta mkokoteni huo walikufa na chombo hicho kuharibika.

Mbali na familia ya Meshack, wengine waliopoteza maisha katika ajali hiyo ni bibi wa miaka 60 (Eveline Masaka) aliyefariki pamoja na mjukuu wake Rehema Yohana na mwingine alikuwa Isack Muhumpha.

Mwili wa Rehema ulichukuliwa na wazazi wake kisha kusafirishwa kwa ajili ya mazishi Chamwino.

Miili sita yazikwa kijijini

Kila kona ya Kijiji ya Manzase ilikuwa ni vilio baada ya miili saba ya marehemu hao kupelekwa Kanisa Anglikana la Mtakatifu Marco kwa ajili ya ibada ya kuwaaga marehemu.

Baada ya ibada hiyo, miili iligawanyika kwa watu kwenda kuzikwa marehemu, huku masanduku matatu yakielekea nyumbani kwa Meshack.

Viongozi washiriki mazishi

Miongoni mwa walioshiriki kwenye mazishi hayo ni mbunge wa Mvumi, Livingston Lusinde (Kibajaji), Katibu Tawala Wilaya ya Chamwino na madiwani wa kata jirani.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *