Televisheni ya Al Mayadeen imeeleza katika ripoti maalumu kuwa, silaha nyingi zilizoingizwa kimagendo nchini Iran kwa ajili ya kutumiika katika vitendo vya kigaidi, kuzusha machafuko na kuvuruga amani zimepitishwa kwa kutumia mpaka wa eneo la Kurdistan ya Iraq.
Kuibuka machafuko hivi karibuni nchini Iran kwa kisingizio cha kifo cha msichana Mahsa Amini kwa mara nyingine tena kumewafanya maadui wa nje wa Jamhuri ya Kiislamu wayatumie machafuko hayo kama fursa ya kuingilia masuala ya ndani ya Iran na kuchochea zaidi machafuko ndani ya nchi.
Katika fujo na machafuko ya hivi karibuni, viongozi wa kisiasa wa Marekani na baadhi wa nchi za Ulaya, vyombo vyao vya habari pamoja na vyombo vya habari vya lugha ya Kifarsi vyenye uadui na Iran vinavyoungwa mkono na nchi za Magharibi, vilitumia kwa maslahi yao tukio la kifo cha Mahsa Amini lililokuwa likiendelea kuchunguzwa, kufanya kila walichoweza kuwaunga mkono wazusha machafuko na wavurugaji usalama kwa kutumia kauli mbiu ya kuunga mkono haki za wananchi wa Iran.
Katika ripoti yake iliyotoa leo, televisheni ya Al-Mayadeen imeelezwa kuwa, maafisa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wanaamini kwamba vitendo vingi vya utumiaji silaha vinavyoshuhudiwa hivi sasa nchini humo chimbuko lake ni eneo la Kurdistan ya Iraq, na ndio maana kuanzia wiki ya kwanza tangu kuanza machafuko hayo, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, IRGC lilivishambulia vituo vya makundi ya kigaidi vilivyoko katika eneo la Kurdistan ya Iraq.
Ripoti hiyo ya Al Mayadeen imeongeza kuwa, viongozi wa Iran wamesisitiza kuwa ikiwa viongozi wa Kurdistan na wa serikali kuu ya Iraq hawatachukua hatua ya kuyapokonya silaha makundi hayo; na kam vikosi vya jeshi la Iraq havitawekwa kwenye eneo la Kurdistan katika mpaka wa nchi mbili, Tehran itaendelea kushambulia makao na vituo vya makundi hayo ya kigaidi.
Jana Jumatatu, vikosi vya makombora na ndege zisizo na rubani vya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu vililenga makao ya makundi ya kigaidi katika mikoa ya Sulaymaniyah na Erbil nchini Iraq.