AMERIKA na Muungano wa Mataifa ya Ulaya (EU) sasa zinalenga mabinti wa kiongozi wa Urusi Vladimir Putin katika juhudi za kumshinikiza kuondoa majeshi yake nchini Ukraine.
Kulingana na ripoti zilizochapishwa Jumatano katika majarida ya Wall Street Journal na Bloomberg, Amerika na EU zinalenga kuwekea vikwazo vya kiuchumi mabinti hao; Maria Vorontsova na Katerina Tikhonova kufuatia hatua ya baba yao, Putin, kutuma wanajeshi kuvamia Ukraine.
Ukraine jana Jumatano iliendelea kupokea msaada wa silaha kutoka mataifa ya Magharibi huku wanajeshi wa Urusi wakiendeleza mapigano makali katika maeneo ya Mariupol na Kharkiv.
Serikali ya Jamhuri ya Czech jana Jumatano ilikuwa nchi ya kwanza ya EU kuipatia Ukraine moja kwa moja silaha za kivita tangu uvamizi wa Urusi uanze siku 42 zilizopita.
Serikali ya Czech ilithibitisha kuwa imetoa msaada wa vifaru aina ya T-72 na magari ya kivita ya BVP-1 kwa Ukraine.
Amerika pia imetangaza kuwa itatoa makombora ya javelin ya thamani ya Sh10 bilioni kwa Ukraine.
Makombora hayo hutumika kukinga au kutungua silaha zinazorushwa na maadui.
Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Amerika Antony Blinken alisema kuwa nchi yake itashirikiana na mataifa rafiki kuhakikisha kuwa wanajeshi wa Urusi walioua halaiki ya watu katika eneo la Bucha, Ukraine, wanaadhibiwa.
Mamia ya miili ya watu ilipatikana katika eneo la Bucha na serikali ya Ukraine inaamini kwamba waliuawa kwa risasi kutoka umbali mfupi.Idara ya ujasusi ya Uingereza jana ilisema kuwa maelfu ya watu wamekwama katika bandari ya Mariupol ambayo imekuwa ikishambuliwa karibu kila siku na majeshi ya Urusi.
“Watu zaidi ya 160,000 wamekwama bandarini hapo na hawana chakula wala umeme,” ikadai ripoti ya kijasusi ya jeshi la Uingereza.
Naibu Waziri Mkuu wa Ukraine Iryna Vereshchuk alisema kuwa juhudi za kuokoa waathiriwa wa vita waliokwama Mariupol zinaendelea.
Vikwazo vipya vilivyotangazwa vinatokana na ghadhabu iliyotokana na mauaji ya Bucha.
Vilifuatia muda mfupi baada ya Rais wa Ukraine Volodomyr Zelenskiy kuhutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC), ambalo lilikutana kujadili mauaji ya halaiki katika mji wa Bucha.
Moscow imekanusha shutuma hizo, ikisema haikuhusika na vifo vya raia ambao maiti zao zilikutwa katika mitaa ya Bucha kaskazini mwa Ukraine.
Zelenskiy pia alilihutubia bunge la Romania, na kusema kuwa idadi ya vifo vya raia katika miji kama vile Borodyanka ni kubwa zaidi kuliko ile ya mjini Bucha.
Kiongozi huyo alisema ni kwa maslahi ya Ukraine kuona kwamba uchunguzi huru unafanyika juu ya uhalifu uliofanyika nchini humo, akiongeza kuwa anahofu kuwa Urusi itajaribu kuharibu ushahidi.
Zelenskiy aliwaalika waandishi wa habari wa kimataifa kufika katika mji wa Bucha na mingineyo nchini Ukraine, kuweka rekodi za uhalifu katika miji iliyokaliwa na jeshi la Urusi.
Vikwazo vingine vilivyowekwa dhidi ya Urusi ni marufuku ya kununua makaa ya mawe kutoka nchi hiyo na kusitisha biashara ya thamani ya Sh2.2 trilioni.
Rais wa Kamisheni ya Ulaya Ursula von der Leyen alisema mataifa ya Ulaya pia yameanza mchakato wa kupiga marufuku mafuta kutoka Urusi.