Amir-Abdollahian: Afrika ni moja ya vipaumbele vikuu vya diplomasia ya kiuchumi ya Iran

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliyeko ziarani nchini Tanzania amesema kuwa, bara la Afrika ni moja ya vipaumbele vikuu vya diplomasia ya kiuchumi ya Iran.

Hussein Amir-Abdollahian amesema hayo leo jijini Dar es Salaam katika kikao cha wanaharakati wa masuala ya kiuchumi na biashara wa Iran na Tanzania ambapo sambamba na kuashiria uwezo wa kiuchumi, kiviwanda na teklojia wa Iran amesisitiza kuwa, Tehran inatoa kipaumbele katika siasa zake za kigeni kuhusu kustawisha uhusiano wa kiuchumi na mataifa ya Kiafrika hususna Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran ameitaja Tanzania kama moja ya nchi muhimu barani Afrika ambayo daima imekuwa na nafasi muhimu katika siasa za kigeni za Tehran na kwamba, wananchi na viongozi wa nchi mbili wana mtazamo chanya baina yao.

Abdollahian ameongeza kuwa, kufanyika kikao cha pamoja cha wanaharakati wa masuala ya kiuchumi na kibiashara wa pande mbili ni ushahidi wa wazi wa hamu na shauku ya pande mbili ya kuinua kiwango cha ushirikiano wa kiuchumi na kwamba, Tanzania ina mazingira mwafaka kwa ajili ya uwekezaji katika sekta mbalimbali kama madini, kilimo, mifugo, uvuvi, viwanda na utalii.

Kadhalika ameeleza kuwa, kuanzishwa kwa Kamishebni ya Pamoja ya Kiuchumi baina ya Iran na Tanzania kwa minajili ya kufuatilia malengo na mipango na vipaumbele baina ya pande mbili kunaweza kuwa hatua moja muhimu na ya  kianzio kwa ajili ya ushirikiano wenye wigo mpana zaidi.

Akiwa jijini Dar es Salaam, Hussein Amir-Abdollahian amekutana na kufanya mazungumzo pia na balozi Liberata Mulamula, Waziri wa Mashauri ya Kigeni na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *