Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu daima itaendelea kuwa pamoja na wananchi wa Yemen.
Hossein Amir-Abdollahian amesema hayo hapa Tehran katika mazungumzo yake na Mkuu wa timu ya mazungumzo ya serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen ambapo pande mbili zimejadiliana masuala ya pande mbili, ya kieneo na ya kimataifa.
Televisheni ya al Alam imetangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, Muhammad Abdu al-Salaam ametembelea Iran kwa mwaliko rasmi na kabla ya kuzungumza na Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, alikuwa ameonana pia na Ali Asghar Haji, Mshauri wa Ngazi za Juu wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika masuala maalumu ya kisiasa na Ali Akbar Velayati, Mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika masuala ya kimataifa. Katika mazungumzo hayo yote, pande mbili zimejadiliana masuala muhimu ya pande mbili, ya kieneo na ya kimataifa.
Muda wote Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikitilia mkazo wajibu wa kutatuliwa mgogoro wa Yemen kwa njia ya mazungumzo na daima imekuwa ikisema kuwa, mgogoro huo kamwe hauwezi kutatuliwa kwa njia za kijeshi.
Mwezi Machi 2015 Saudi Arabia kwa kushirikiana na baadhi ya nchi za Kiarabu hasa Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) zilianzisha mashambulio ya pande zote dhidi ya nchi maskini zaidi ya Kiarabu ya Yemen kwa baraka kamili na kwa misaada ya kila upande ya madola ya Magharibi hasa Marekani.
Tangu wakati huo hadi hivi sasa madola hayo vamizi yameizingira kila upande Yemen, kutokea ardhini, angani na majini.
Pamoja na hayo na tofauti kabisa na ndoto walizokuwa nazo wavamizi wa Yemen, wananchi wa taifa hilo la Kiislamu wamesimama imara kujihami na kuilinda nchi yao kwa zaidi ya miaka 7, wametoa vipigo vikali kwa wavamizi hasa Saudia kwa kushambulia maeneo yao nyeti kama shirika la mafuta la Aramco na kuwakwamisha wavamizi hao katika kinamasi kizito.