Amir-Abdollahian: Iran itamteua balozi wake Saudi Arabia hivi karibuni

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian anasema hivi karibuni kwamba Iran itamteua balozi wake huko Saudi Arabia huku nchi hizi mbili zikiwa katika mchakato wa kurejesha uhusiano wa kawaida kufuatia makubaliano yaliyofikiwa huko China mwezi Machi uliopita.

Amir-Abdollahian ameyasema hayo katika mahojiano na ICANA, shirika la habari linalofungamana na Bunge la Iran, yaliyochapishwa Jumatano.

Amebainisha kuwa maelezo zaidi ya kufunguliwa tena ubalozi wa Saudia mjini Tehran yatatangazwa hivi karibuni.

Amir-Abdollahian ameongeza kuwa, kurejeshwa uhusiano kati ya Iran na Saudi Arabia kutaibua “uwezo mkubwa” ambao unaweza kuhudumia maslahi ya nchi hizi mbili, kanda na ulimwengu wa Kiislamu.

Matamshi hayo yametolewa wakati mawaziri wa mambo ya nje wa mataifa hayo mawili wakifanya mkutano wao wa kwanza katika kipindi cha miaka saba mjini Beijing tarehe 6 Aprili, wakisisitiza haja ya kutekelezwa makubaliano ya maridhiano yaliyotiwa saini tarehe 10 Machi.

Akizungumza siku ya Jumatatu katika mkutano wake wa kila wiki na waandishi wa habari, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Nasser Kan’ani amesema “maendeleo mazuri” yamepatikana katika mchakato wa kufunguliwa tena kwa balozi za kidiplomasia.

Kulingana na makubaliano na uamuzi wa kiutendaji, tumekuwa na maendeleo mazuri katika mchakato wa kufungua balozi,” amesema, akiongeza kuwa “muda zaidi” unahitajika kwa sababu majengo hayajatumika kwa miaka mingi.

Wajumbe wa kiufundi kutoka Tehran na Riyadh tayari wametembelea balozi za kidiplomasia katika wiki zilizopita ili kufanya mpangilio unaohitajika na maandalizi ya kufunguliwa tena.

Iran na Saudi Arabia zilikubali kurejesha uhusiano wao wa kidiplomasia na kufungua tena balozi zao baada ya siku kadhaa za mazungumzo mazito yaliyoandaliwa na China mnamo Machi 10.

Katika taarifa ya pamoja baada ya makubaliano hayo, Tehran na Riyadh zilisisitiza umuhimu wa kuheshimu mamlaka ya kitaifa ya kila mmoja na kuepuka kuingiliwa masuala ya ndani ya upandfe wa pili.

Pia zilikubaliana kutekeleza makubaliano ya ushirikiano wa kiusalama kuanzia Aprili 2001 na makubaliano mengine kuanzia Mei 1998 ili kuimarisha ushirikiano wao katika nyanja mbalimbali, kama vile uchumi, biashara, uwekezaji, teknolojia, sayansi, utamaduni, michezo na masuala ya vijana.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *