Amir-Abdollahian: Oman ina ubunifu mzuri kuhusu kadhia ya nyuklia ya Iran

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, serikali ya Oman ina ubumifu mzuri kuhusu kadhia ya nyuklia ya Iran, ubunifu ambao utasaidia kurejea mazungumzo katika suala hilo.

Hossein Amir-Abdollahian amesema hayo akiwa ziarani nchini Oman jana Jumanne ambapo alipokewa na waziri mwenzake wa mambo ya nje wa Oman na viongozi wengine wa ngazi za juu wa nchi hiyo ya Kiarabu.

Serikali ya 13 ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeelekeza nguvu zake kwenye kuimarisha uhusiano wa kikanda hasa na nchi za eneo hili la Asia Magharibi.

Akihojiwa na shirika rasmi la habari la Oman, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amemshukuru Sultan Haitham bin Tariq Aal Said wa Oman na serikali ya nchi hiyo kutokana na mchango wake mzuri wa kuhakikisha vikwazo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vinaondolewa. Amesema, jitihada za Muscat katika suala hilo zina matunda mazuri.

Aidha amesema kuhusu mazungumzo yake na waziri mwenzake wa mambo ya nje wa Oman, Badr bi Hamad Albusaidi kwamba, katika mazungumzo hayo wamejadiliana masuala muhimu ya ushirikiano wa pande mbili, masuala ya kieneo na kimataifa hasa kadhia ya Palestina, hali ya Sudan pamoja na juhudi za kuleta upatanishi nchini Yemen kwa kuwatumia Wayemen wenyewe.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran pia amesema, ushirikiano wa nchi yake na Oman umeongezeka saina hivi sasa hasa katika masuala ya kiuchumi na uwekezaji.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *