Hossein Amirabdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema katika kikao na kundi la viongozi na wanachama mashuhuri wa makundi mbalimbali ya mapambano ya Palestina kwamba Palestina na Quds Tukufu bado ni suala la kwanza la ulimwengu wa Kiislamu.
Hossein Amirabdollahian, akiendelea na safari yake nchini Syria, alikutana na kuzungumza na idadi kubwa ya viongozi na wanachama mashuhuri wa makundi mbalimbali ya muqawama wa Palestina mjini Damascus, Jumamosi usiku.
Amir Abdollahian amesisitiza katika kikao hicho kwamba Palestina na Quds Tukufu bado ni suala la kwanza la ulimwengu wa Kiislamu hadi pale taifa la Palestina litakapoundwa katika ardhi ya kihistoria ya Palestina mji mkuu wake ukiwa ni Quds Sharif.
Amesema kufanyika mkutano huo katika mji mkuu wa Syria ambapo viongozi na wawakilishi mashuhuri wa makundi ya muqawama wa Palestina wamehudhuria ni dalili ya kuwepo mshikamano na umoja kati ya viongozi hao katika kuiunga mkono Palestina.
Mkuu huyo wa chombo cha diplomasia ya Iran amesema Marekani na washirika wake wamewasilisha mipango mbalimbali ya hadaa moja baada ya mwingine kwa miaka mingi, ikiwemo ya Oslo, Mashariki ya Kati Mpya, Mashariki ya Kati Kuu, Makubaliano ya Karne na Mkataba wa Abraham, lakini taifa na mrengo wa mapambano wa Palestina umedhihirisha umoja, mshikamano na ukakamavu wake wa kupigiwa mfano, na hatimaye kusambaratisha mipango yote hiyo na kuitupa kwenye jaa la taka la historia.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameongeza kuwa, operesheni ya “Upanga wa Quds” imethibitisha wazi kuwa muqawama na Palestina zingali ziko hai.
Ameendelea kusema kuwa hata Kombe la Dunia la Qatar limethibitisha wazi karibuni kuwa Palestina ingali iko hai na kwamba juhudi za baadhi ya nchi za Kiarabu za kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala ghasibu wa Israel hazina thamani yoyote.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran ameeleza kuwa, kubadilishwa majina na nyuso za watawala katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu hakubadilishi chochote, bali viongozi wa utawala wa Kizayuni wanahama kutoka itikadi moja kali hadi nyingine kali zaidi, jambo ambalo linatokana na matatizo na migogoro mikubwa ya kiusalama na kijamii ndani ya Israel.
Amesisitiza kuwa, bila shaka watu wenye misimamo mikali ndani ya utawala huo ghasibu wanaimarisha umoja na mshikamano katika mrengo wa muqawama na taifa la Palestina.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran aliondoka Lebanon kuelekea Syria siku ya Jumamosi.
Ikumbukwe kuwa Hossein Amirabdollahian, aliwasili mjini Beirut Alkhamisi usiku kwa mwaliko wa waziri mwenzake wa Lebanon na siku ya Ijumaa alikutana na kuzungumza na viongozi wa Lebanon akiwemo Waziri Mkuu, Waziri wa Mambo ya Nje, Spika wa Bunge na Katibu Mkuu wa Hizbullah, Sayyid Hassan Nasrullah.