Amnesty International: Ghasia kubwa za Sudan Kusini zinaweza kuwa uhalifu wa kivita

Ripoti iliyotolewa na shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International imesema kuwa kuongezeka kwa mapigano kati ya makundi hasimu yenye silaha yanayoshirikiana na serikali na vikosi vya upinzani nchini Sudan Kusini mwaka huu kumeua makumi ya raia na kuibua “vurugu zisizotasawarika” ambazo zinaweza kuwa uhalifu wa kivita.

Faraan: Katika ripoti yake mpya iliyotolewa Alhamisi, Amnesty International imesema wapiganaji wa pande zote zinazozozana wameharibu vijiji vizima kiholela wakati wa mapigano ya kati ya Juni na Oktoba katika jimbo la Equatoria Magharibi ambayo pia yaliwalazimisha makumi ya maelfu ya raia kukimbia makazi yao.

Amnesty imesema imesajili matukio yanayoweza kutambuliwa kuwa ni uhalifu wa kivita na ukiukaji mwingine unaofanywa na pande zinazopigana dhidi ya watu wa jamii za Azande na Balanda.

Mkurugenzi wa Amnesty International kanda ya Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika, Deprose Muchena amesema kuwa: “Mfululizo wa vifo, uharibifu na migawanyiko ilitokea baada ya wanasiasa kuchochea chuki za kikabila na kuwahamasisha vijana kupigana. Ushahidi tuliokusanya unaeonesha ukatili usiotasawarika ikiwa ni pamoja na kuuliwa raia waliokuwa wakikimbia na miili kuchomwa moto na kukatwa viungo.”

Sudan Kusini yenye utajiri wa mafuta ilipata uhuru mnamo Juni 2011 lakini imekumbwa na ghasia na machafuko ya kikabila tangu Disemba 2013 wakati vikosi vinavyomtii Rais Salva Kiir vilipoanza kupambana na waasi waliokuwa wakiongozwa na naibu wake, Riek Machar. Vita hivyo vya wenyewe kwa wenyewe vimeua karibu watu 400,000 na kuwalazimisha mamilioni na wengine kuwa wakimbizi.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *