Amnesty International: Marekani inapasa kufuta doa la Guantamano

Sambamba na maadhimisho ya kutimia mwaka wa 21 tangu kuanza kazi gereza la Guantanamo huko katika Ghuba ya Cuba; Shirika la Msamaha Duniani (Amnesty International) limelaani jinai za miaka 21 katika gereza hilo zilizotekelezwa na Wamarekani.

Tarehe 11 Januari mwaka 2002 jela za kijeshi zilizokuwa chini ya ulinzi mkali sana katika kambi ya jeshi la majini la Marekani katika Ghuba ya Cuba zilianza kazi; ambapo wale wote ambao walitiwa nguvuni katika vita vilivyodaiwa na rais wa wakati huo wa Marekani George Bush eti dhidi ya ugaidi walipasa kufungwa jela na kuhukumiwa nje ya Marekani.

Erica Guevara-Rosas, Mkurugenzi wa Amerika wa Amnesty International ameeleza kuwa, inasikitisha kwamba miaka 21 baada ya kufunguliwa gereza la  Guantanamo; tena hiyo ikiwa ni kwa kukiukwa sheria, Marekani inaendelea kuwashikilia watu 35 katika jela za gereza hilo. Afisa huyo wa Amnesty International ameongeza kuwa, akthari ya watuhumiwa hao 35 hawajawahi kuhukumiwa kwa kosa au uhalifu wowote.

Erica Guevara Rosas ameeleza kuwa, tume ya kijeshi iliyoundwa kuchunguza kesi za baadhi ya watuhumiwa hao si ya kiadilifu na haiwajibiki. Tume hiyo haiwapi haki watuhumiwa ya kuwa na wakili wa kuwatetea.

Amnesty International imemtaka Rais Joe Biden wa Marekani awahamishie haraka wafungwa ambao hawajawahi kuhukumiwa katika nchi ambazo watakuwa salama na ambazo zinaheshimu haki za binadamu. Mkurugenzi wa Amerika wa Amnesty International aidha amesisitiza kuwa, Guantanamo bado ni doa katika historia ya Marekani. Miongo miwili imepita sasa tokea kufunguliwa kwa gereza hilo linalopatikana katika Ghuba ya Cuba; gereza ambalo linapasa kufungwa milele daima.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *