Ansarullah yakataa kushiriki katika kikao cha Riyadh

Harakati ya wananchi wa Yemen ya Ansarullah imetaa ombi la Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi la kwenda Riyadh na kufanya mazungumzo na Saudi Arabia.

 Miaka 7 imepita tangu Saudi Arabia ianzishe vita dhidi ya taifa la Yemen. Al-Saud ambao walitarajia kushinda vita hivyo kwa muda mfupi, sasa wamekwama kwenye kinamasi cha Yemen. Vita hivi pia vimekuwa na gharama kubwa za kiuchumi na kisiasa kwa Saudi Arabia. Wakati huo huo, sura na hadhi ya kijeshi na kisiasa ya Saudi Arabia imeporomoka kutokana na kurefuka kwa vita hivyo; kwani haijaweza kupata ushindi wa kijeshi dhidi ya nchi hiyo masikini na dhaifu zaidi za Kiarabu.

Hadi sasa kumefanyika juhudi nyingi kwa ajili ya kukomesha vita hivyo, haswa zile za wajumbe wa Umoja wa Mataifa, lakini hazijazaa matunda. Moja ya sababu za kushindwa juhudi za kukomesha mgogoro wa Yemen ni msimamo wa Saudi Arabia wa kukataa kuitambua rasmi harakati ya wananchi wa Yemen ya Ansarullah na Serikali ya Uokovu wa Taifa ya Yemen. Hata hivyo baadhi ya maafisa wa nchi za Kiarabu katika Baraza la Ushirikiano wa Ghuba ya Uajemi hivi karibuni walitangaza kuwa, baraza hilo limeamua kuzialika pande husika katika mgogoro wa Yemen kwenye kikao nchini Saudi Arabia. Mwaliko huo umekataliwa na harakati ya Ansarullah na maafisa wa Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen.

Kuna sababu kadhaa za msimamo huo wa Ansarullah na Serikali ya Uokovu. Kwanza ni kuwa Baraza la Ushirikiano wa Ghuba ya Uajemi (PGCC) limekuwa likipendelea upande mmoja katika mgogoro wa Yemen, na daima limekuwa likiunga mkono serikali iliyojiuzulu ya Sana’a na Saudi Arabia. Kwa hivyo, kimsingi, baraza hili ambalo nchi mbili za Saudi Arabia na Imarati (UAE) zinazopigana na Yemen ni miongoni mwa wanachama wake, haliwezi kuwa mwenyeji wa mazungumzo kati ya pande zinazohusika.

Pili ni kwamba kikao cha Baraza la Ushirikiano wa Ghuba ya Uajemi kitafanyika mjini Riyadh. Ikiwa maudhui ya kikao hicho ni upatanishi kuhusu mgogoro wa Yemen, basi kikao hicho kinapaswa kufanyika katika nchi isiyopendelea upande wowote, na sio nyumbani kwa mhusika mkuu katika mgogoro huo.

Kuhusiana na hilo, Muhammad Ali al-Houthi, mjumbe wa ngazi ya juu wa Idara ya Siasa ya harakati ya Ansarullah ya Yemen anasema: “Kinachosemwa kwenye vyombo vya habari kuhusu mwaliko wa Baraza la Ushirikiano wa Ghuba ya Uajemi kwa ajili ya mazungumzo kwa hakika ni ombi la Riyadh ambayo yenyewe ni sehemu ya vita, si mpatanishi.”  Hisham Sharaf, Waziri wa Mambo ya Nje wa Serikali ya Uokovu wa Taifa ya Yemen pia amesema: “Baraza la Ushirikiano, Abu Dhabi na Riyadh, ambayo ni mwenyeji wa mkutano huu, ndio sababu kuu ya vita na kuzingirwa kwa Yemen; hivyo na sio busara pande hizo kuwa wapatanisha katika mgogoro huu.”

Msimamo wa Ansarullah na Serikali ya Uokoaji wa Kitaifa ya Yemen wa kukataa mwaliko wa Riyadh wa kuhudhuria kikao cha PGCC ni hatua ya kimantiki, kwa sababu mazungumzo yatakuwa na tija pale kutakapokuwepo irada na azma ya kweli ya kukomesha mgogoro huo. Hii ni pamoja na kuwa, mazungumzo yanayofanyika wakati Saudia na washirika wake wakiendeleza mashambulizi ya kila siku na mauaji ya raia wasio na hatia na vilevile mzingiro wao wa kidhalimu dhidi ya Yemen, hayawezi kuwa na matunda.

Katika uwanja huo Hisham Sharaf, Waziri wa Mambo ya Nje wa Serikali ya Uokoaji wa Kitaifa ya Yemen amesema: “Saudi Arabia na UAE zinapaswa kwanza kufungua tena uwanja wa ndege wa Sanaa, kupunguza mzingiro, kuruhusu uingizaji wa bidhaa za mafuta na gesi, na kukomesha mashambulizi dhidi ya Yemen kabla ya suluhisho lolote la kisiasa.”

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *