Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema ofisi yake inafanya jitihada zote ili kutatua mgogoro wa Ukraine bila umwagaji zaidi wa damu.
Akizungumza mjini New York, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa, kuna haja ya kukutana na kukabiliana na changamoto hii pamoja kwa ajili ya amani, na kuokoa watu wa Ukraine ili waondokane na janga la vita.
Amesema yeye pamoja na ofisi yake wanajitolea, “kikamilifu kwa jitihada zote kutatua mgogoro huu bila umwagaji zaidi wa damu. Ninarudia: Ofisi zangu nzuri ziko na hatutalegea katika kutafuta suluhu ya amani. Umoja wa Mataifa na mfumo mzima wa kimataifa unajaribiwa. Ni lazima tushinde jaribio hili.”
Huku akikosoa hatua ya Russia ya kutambua uhuru wa mikoa ya Donetsk na Luhansk ya Ukarine Guterres amesema Jumanne amelazimika kukatisha “ziara ya nje ya nchi ikiwa ni pamoja na mkutano muhimu sana wa viongozi wa Afrika ili kurejea makao makuu ya Umoja wa Mataifa.”
Amesema, “ulimwengu wetu unakabiliwa na mzozo mkubwa zaidi wa amani na usalama duniani katika miaka ya hivi karibuni.
Rais Vladimir Putin wa Russia juzi alitangaza kuwa nchi yake imetambua rasmi uhuru wa Jamhuri za watu wa Donetsk na Luhansk na tayari amesaini mikataba ya ushirikiano na urafiki na viongozi wa jamhuri mbili hizo katika ikulu ya Kremlin.
Kufuatia hatua hiyo ya Russia, Baraza la Usalama la UN limefanya kikao cha dharua kujadili suala hilo Jumatatu.
Wakati huo huo Marekani imefuta mkutano ambao ilikuwa imeitisha baina ya waziri wake wa mambo ya Nje Antony Blinken na mwenzake wa Russia Sergey Lavrov Alhamisi mjini Geneva. Marekani imedai imefuta mkutano huo kutokana na hatua ya Russia kutuma askari wake katika maeneo ya Ukraine ambayo yamejitangazia uhuru na kutambuliwa rasmi na Moscow.