Katika ufichuzi wa kutatanisha, ripoti ya hivi punde ya Shirika la Umoja wa Matafa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO, imefichua kuwa asilimia 29 watoto wa umri wa kwenda shule barani Afrika bado wananyimwa fursa ya kupata elimu.
Takwimu hii “ya kutisha” inaashiria tatizo kubwa katika bara hili, kwani idadi ya watoto ambao hawakuwa shuleni ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara barani Afrika iliongezeka kwa milioni 12 kati ya 2015 na 2021.
Ripoti hiyo, iliyotolewa kwa pamoja na UNESCO na UNICEF katika Siku ya Kimataifa ya Elimu, inafichua zaidi ukweli unaotia wasiwasi: asilimia 90 ya watoto katika eneo hilo la kusini mwa Jangwa la Sahara hawawezi kusoma na kuelewa maandishi ya msingi kufikia umri wa miaka 10.
Tasisi za UNICEF na UNESCO zimeahidi kushirikiana na serikali za Afrika, kutetea upatikanaji wa elimu bora kwa kila mtoto.
Taarifa ya pamoja ya mashirika hayo mawili ya Umoja wa Mataifa inazipongeza serikali za Afrika kwa uongozi wao katika kujadili masuluhisho ya kupata elimu jumuishi na yenye usawa wakati wa Mkutano wa Mabadiliko ya Elimu.
Licha ya hatua kubwa zilizopigwa katika miongo ya hivi karibuni, changamoto zinazoendelea zinatishia kufikiwa kwa Lengo la 4 la Maendeleo Endelevu kuhusu elimu lililoainishwa katika Ajenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu. Taarifa hiyo inazitaka serikali na washirika kuweka kipaumbele cha elimu katika ajenda ya kisiasa, ikisisitiza haja ya ufadhili wa haki wa kitaifa wa umma.
Taarifa hiyo mpya imepelekea kutiliwe mkazo umuhimu wa juhudi endelevu za kushughulikia mzozo wa elimu barani Afrika, kuhakikisha kuwa vijana wa bara hili wanakuwa na zana kwa ajili ya maisha bora ya baadaye.