Wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel wamewaua shahidi watoto Wapalestina zaidi ya 2,000 tokea mwaka 2000
Faraan: Hayo yamedokezwa na Khaled Quzmar Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la Kutetea Watoto Wapalestina na kuongeza kuwa, baada ya vita vya mwaka 2014 ambavyo viliendelea Ghaza kwa muda wa siku 50, idadi kubwa ya watoto Wapalestina wameuawa shahidi katika mwaka 2021.
Ripoti hiyo imeongeza kuwa, katika mwaka huu wa 2021, watoto 86 Wapalestina wameuawa shahidi katika hujuma za wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel na walowezi wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi, Quds (Jerusalem) na Ghaza. Aidha amesema katika vita vya siku 12 Ghaza mwaka huu, watoto 67 Wapalestina waliuawa shahidi.
Aidha tokea mwanzo wa mwaka huu, watoto 15 Wapalestina wamekufa shahidi baada ya kufyatuliwa risasi na askari wa utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukingo wa Magharibi na watoto wengine wawili wamepoteza maisha baada ya kushambuliwa na walowezi wa Kizayuni katika eneo hilohilo.
Wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel huwaua watoto Wapalestina kiholela katika hatua ambayo ni jinai ya wazi dhidi ya binadamu.
Hayo yanajiri wakati ambao Harakati za Palestina za HAMAS na Jihadul-Islami zimetahadharisha kuwa eneo la Ukanda wa Ghaza linakabiliwa na hali mbaya sana ya kibinadamu kutokana na mzingiro wa kinyama liliowekewa na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel.