Askofu Mkuu wa Kanisa la Othodoksi mjini Baitul Muqaddas (Jerusalem) amesema: Palestina haitafunga mikono na kusimama kizembe katika kukabiliana na upendeleaji unaofanywa na Magharibi kwa utawala ghasibu wa Kizayuni pamoja na sera na jinai zake.
Marekani ndiyo muungaji mkono mkubwa zaidi wa jinai za utawala wa Kizayuni katika eneo la Magharibi mwa Asia, jambo ambalo linaushajiisha utawala huo dhalimu kushadidisha jinai zake hizo. Mpango wa kibaguzi uliopewa jina la Muamala wa Karne, kuidhinishwa msaada wa dola bilioni 38 za Marekani kwa utawala wa Kizayuni na baadae kukatwa msaada wa kifedha wa Marekani kwa Shirika la Misaada na Ajira kwa Wakimbizi wa Kipalestina UNRWA ni baadhi tu ya mifano ya uungaji mkono huo wa serikali ya Washington kwa utawala ghasibu na haramu wa Israel.
Kwa mujibu wa chaneli ya televisheni ya Al-Mayadeen, Attaullah Hana, Askofu Mkuu wa Kanisa la Othodoksi katika mji wa Quds unaokaliwa kwa mabavu amesema: “jinai za utawala wa Kizayuni hazitasahaulika kwa sababu ya muda kupita, na tunafahamu vyema jinsi jamii ya kimataifa inavyoupendelea utawala wa Kizayuni.”
Hana ameongezea kwa kusema: “Wapalestina hawatafunga mikono kutazama tu upendeleo unaofanywa na Magharibi kwa utawala unaoikalia Quds kwa mabavu pamoja na sera na jinai zake, bali wataendeleza muqawama na kushikamana na misingi na piganio lao.”
Askofu Mkuu wa Kanisa la Othodoksi katika mji wa Baitul Muqaddas unaokaliwa kwa mabavu amesisitiza kuwa, Wapalestina hawana hofu ya chochote; na kwamba jinai zote hizo, njama pamoja na mauaji hayatakuwa na natija yoyote isipokuwa kushikamana zaidi Wapalestina na piganio lao la haki na uadilifu la kadhia ya Palestina, haki yao ya kihistoria, kikaumu na kitaifa katika ardhi hiyo na kuthibitisha kwamba ardhi ya Palestina ni milki ya Wapalestina.