Rais wa Syria Bashar al-Assad amekosoa misimamo ya kundumakuwili ya nchi za Magharibi katika kukabiliana na wahanga wa mitetemeko mikubwa ya ardhi iliyokumba Syria na Uturuki, akisema mataifa ya Magharibi hayajali hali ya kibinadamu nchini kwake.
Assad aliyasema hayo Ijumaa katika hotuba yake wakati alipotembelea maeneo yaliyokumbwa na tetemeko la ardhi.
Rais Assad amesema, “Unduakuwili wa nchi za Magharibi sio jambo jipya na umekuwepo tangu karne sita zilizopita.”
Aidha amewaahidi wananchi kuwa “atafanya kazi bila kukoma” kusaidia wahasiriwa wa mitetemeko ya ardhi na kupunguza shida zao iwezekanavyo.
“Rais huwa hatumi ujumbe kwa wananchi, bali anapokea ujumbe kutoka kwa wananchi na ujumbe wetu ni kazi ya dhati na ya uadilifu,” amesema.
Assad pia amesema “Wasyria hawazungumzi, wanachukua hatua,” akiongeza kuwa watu wa nchi yake wamekabiliana na matatizo katika kipindi cha miaka 12 iliyopita huku wakizingatia maadili yao na watafanikiwa katika kukabiliana na janga hili la kimaumble pia.
Assad na mkewe walitembelea Aleppo kuangalia shughuli za uokoaji siku ya Ijumaa. Pia walikutana na watu waliojeruhiwa katika mitetemeko hiyo ya ardhi.
Matetemeko hayo mabaya ya ardhi yalikumba Uturuki na nchi jirani ya Syria mapema Jumatatu. Mtetemeko huo wa kipimo cha 7.8 hadi sasa umeua zaidi ya watu 30,000 kwa jumla katika nchi hizo mbili.
Wito unazidi kuongezeka kwa Marekani na washirika wake kuondoa vikwazo vyao dhidi ya Syria, jambo ambalo maafisa na wahudumu wa misaada mashinani wanasema vinatatiza juhudi za misaada ya kimataifa nchini humo.
Tetemeko la kwanza la ardhi la ukubwa wa 7.8 katika kipimo cha Rishta lilitikisa kusini mwa Uturuki na kaskazini mwa Syria Jumatatu asubuhi ya tarehe 6 Februari. Kitovu chake kilikuwa ni katika mji wa Gaziantep wa Uturuki ambapo mamia ya majengo yameporomoka.Masaa machache baadaye kulijiri mtetemeko mwingine wa ardhi uliokuwa na ukubwa 7.6 kwenye kipimo cha rishta.