Athari mbaya za vita vya Yemen kwa wanawake na watoto

Waziri wa Afya wa serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen amesema kuwa, wanawake na watoto wa nchi hiyo ndio wanaoathiriwa moja kwa moja na athari mbaya za vita vya Saudi Arabia na washirika wake dhidi ya nchi hiyo.

Saudi Arabia ikiungwa mkono na Marekani, Imarati na nchi nyingine kadhaa, mwezi Machi 2015 ilianzisha vita dhidi ya Yemen na kuiwekea nchi hiyo mzingiro wa nchi kavu, baharini na anga.

Vita vya Saudia na waitifaki wake huko Yemen hadi sasa vimeuwa maelfu ya raia wasio na hatia na kujeruhi makumi ya maelfu ya wengine, huku mamilioni ya Wayemeni wakilazimika kuwa wakimbizi.

Televisheni ya al Masira imeripoti kuwa, Dakta Taha al Mutawakkil, Waziri wa Afya wa Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen ameeleza kuwa, wanawake na watoto wa nchi hiyo wanakabiliwa moja kwa moja na athari mbaya za vita; jambo ambalo kwa muda mrefu litasababisha taathira za kisaikolojia na kimwili. Dakta al Mutawakkil ameongeza kusema kuwa, vita dhidi ya Yemen imeuwa watoto na wanawake zaidi ya elfu nane katika muda wa miaka minane iliyopita.

Waziri wa Afya wa Yemen amesisitiza kuwa, jinai za muungano vamizi wa Saudia zingali zinaendelea na hili linadhihirika kufuatia kuongezeka matatizo ya kijenetiki kutokana na mashambulizi na hujuma za mabomu ya vishada dhidi ya raia wa Yemen.

Dakta al Mutawakkil ameliomba Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) kupaza sauti katika duru za kimataifa kuhusu kiwango kikubwa cha maafa yanayowasibu watoto wa Kiyemeni.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *