Ayatullah Khamenei: Ayatullah Golpaygani alikuwa miongoni mwa nembo na nguzo muhimu katika chuo kikuu cha kidini cha Qum

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei ametuma ujumbe wa salamu za rambirambi kutokana na kifo cha mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu, Ayatullah Safi Golpaygani aliyeaga dunia usiku wa kuamkia leo.

Ujumbe wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu unaeleza kuwa: Ayatullah Safi Golpaygani alikuwa mmoja kati ya nguzo za chuo kikuu cha Qum (Hauza) na miongoni mwa vinara wa elimu na amali, na mmoja kati ya wanazuoni wazoefu zaidi wa kidini.

Katika ujumbe wake, Kiongozi wa Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Katika zama za hayati Ayatullah Boroujerdi, Ayatullah Safi Golpaygani alikuwa akihesabiwa kuwa miongoni mwa wanafunzi hodari wa mwalimu huyo mkubwa, na alikuwa sahiba na mshauri wa hayati Ayatullah Sayid Muhammad Reza Golpaygani. Amesema katika kipindi chha baada ya Mapinduzi ya Kiislamu, alikuwa mtu aliyetegemewa na kuaminiwa na Imam Khomeini, Mungu awarehemu.

Ayatullah Khamenei ameongeza katika ujumbe wake kuwa: “Ayatullah Safi Golpaygani alikuwa miongoni mwa nguzo kuu za Baraza la Walinzi wa Katiba kwa miaka mingi, na baada ya hapo alishughulikia masuala ya mapinduzi na nchi kwa moyo wa kuwajibika na alinipa ushauri na kunieleza mitazamo na maoni yake mara kwa mara.”

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekitaja kipaji cha ushairi, uwezo mkubwa wa kumbukumbu za kihistoria na kushughulikia masuala ya kijamii kuwa ni miongoni mwa sifa za shakhsia ya mwanazuoni huyo mkongwe na adhimu, ambaye amesema kifo chake ni hasara kubwa kwa jamii ya kielimu na kidini hapa nchini.

Ayatullah Ali Khamenei ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya msom huyo na watoto wake, na vilevile kwa marajii na maulama wakubwa wa chuo kikuu cha kidini cha Qum (Hauza), na wafuasi wake hususan katika miji ya Qum na Gopaygani. Vilevile amemuombea rehma na maghufira ya Mwenyezi Mungu.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *