Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limeunga mkono kwa wingi mkubwa mno wa kura azimio la kuutaka utawala haramu wa Kizayuni wa Israel uachane na silaha zake za nyuklia na kujiunga na Mkataba wa Kuzuia Uundaji na Uenezaji Silaha za Nyuklia (NPT).
Katika mkutano wa Baraza Kuu la UN, nchi 149 wanachama wa Umoja wa Mataifa zimepiga kura ya ‘ndiyo’ huku sita tu zikipinga rasimu ya azimio ambalo toleo lake la awali liliidhinishwa katika Kamati ya Tano ya Baraza Kuu mwezi Oktoba kwa kura 152 dhidi ya kura tano zilizopinga.
Azimio hilo limeitaka Israel “kutotengeneza, kutozalisha, kutozifanyia majaribio wala kusaidia wengine kupata silaha za nyuklia” na “kuachana na umiliki wa silaha za nyuklia.”
Azimio hilo la Baraza Kuu la UN limetoa wito pia kwa utawala haramu wa Israel kuukubali mkataba wa NPT na kuweka vituo vyake vyote vya nyuklia chini ya usimamizi kamili wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, IAEA.
Kanada, Israel, Micronesia, Palau na Marekani zimepiga kura kupinga azimio hilo. Liberia, ambayo ilikuwa haijashiriki katika upigaji kura mwezi Oktoba, imebadilisha msimamo wake na kupiga kura ya ‘hapana’.
Azimio hilo Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipendekezwa Palestina na nchi 20, wakiwemo washirika wa utawala wa Kizayuni wa Israel katika Asia Magharibi walioanzisha uhusiano wa kawaida na utawala huo, ambao ni Misri, Jordan, Bahrain, Morocco, Sudan na Muungano wa Falme za Kiarabu.
Israel inajulikana kuwa ndio utawala pekee unaomiliki silaha za nyuklia katika eneo la Asia ya Magharibi, lakini haijawahi kukiri rasmi kuwa na silaha hizo.
Utawala huo wa Kizayuni na nchi za India, Pakistan na Sudan Kusini ndizo ambazo hadi sasa hazijasaini Mkataba wa Kuzuia Uundaji na Uenezaji Silaha za Nyuklia (NPT)