Wabunge na maseneta wateule nchini Kenya wanatarajiwa kufanya vikao vyao vya kwanza kabisa siku ya Alkhamisi ya wiki hii, Septemba 8, 2022 siku chache baada ya Mahakama ya Juu ya nchi hiyo kutupilia mbali mashitaka ya mgombea urais Raila Odinga na kudhibitisha ushindi wa Dk William Ruto kama ulivyotangazwa na tume ya uchaguzi ya IEBC.
Tangazo la kufanyika vikao hivyo limetolewa baada ya Rais Uhuru Kenyatta wa nchi hiyo kuchapisha ilani katika gazeti rasmi la serikali ya kuitisha vikao vya kwanza vya Bunge la 13 baada ya uchaguzi mkuu uliofanyika Agosti 9.
Vikao hivyo, vitafanyika katika kumbi za mabunge hayo zilizoko katika majengo ya bunge, jijini Nairobi kuanzia saa tatu asubuhi kwa majira ya Afrika Mashatiki.
Wakati huo huo Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC) Bw Wafula Chebukati amesema kuwa, tume yake iliweka mifumo imara ya kuhakikisha kunakuwa na uadilifu katika uchaguzi mkuu uliopita.
Akizungumza kwa mara ya kwanza baada ya kumtangaza Naibu Rais William Ruto kuwa Rais Mteule, Chebukati amesema, tume yake ilifanikisha uchaguzi huo kwa kiwango cha hali ya juu licha ya vitisho na baadhi ya wafanyakazi wa IEBC kuuawa wakiwa kazini.
Alisema kwamba wafanyakazi wa IEBC walikamatwa kiholela, wakatekwa nyara na kuteswa na watu wanaoaminika walitoka idara za usalama.
Bw Chebukati amewashukuru Wakenya kwa kutekeleza haki zao za kidemokrasia kwa kupiga kura mnamo Agosti 9 mwaka huu kwa utulivu na usalama.
Alisema: “Tuliweka mifumo thabiti kuhakikisha uchaguzi ulikuwa huru. Uchaguzi ni mchakato na sio tukio la siku moja. Tumeondolewa lawama na Mahakama kwa kuamua kwamba tulifanya uchaguzi huru, haki na wa uwazi.”